• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 5:50 AM
CORONA: Huduma za feri kusimamiwa na polisi

CORONA: Huduma za feri kusimamiwa na polisi

Na MOHAMED AHMED

RAIS Uhuru Kenyatta ameamrisha jeshi la baharini pamoja na maafisa wa polisi kuchukua usukani wa huduma za kivuko cha Likoni.

Akizungumza jana jioni, Rais Kenyatta alisema kuwa ili kuweka mikakati ya kuzuia kusambaa kwa virusi vya corona katika feri, maafisa hao wa usalama wameamrishwa kusaidia katika uchukuzi wa watu na magari.

“Kuanzia sasa. Huduma za feri zimepatiwa maafisa hao wa usalama na wao ndio wataelekeza mipango ya huduma hizo kivukoni hapo. Maafisa hao ndio watakaotoa maelezo zaidi wakiwa hapo,” akasema Rais Kenyatta.

Kivuko cha hicho cha feri hutumiwa na watu zaidi ya 320,000 na magari 6,000 kila siku ambao wameendelea kuvuka licha ya mkurupuko wa virusi vya korona.

Hapo awali, Wizara ya Uchukuzi ilikuwa imetoa agizo kwa KFS kuwa watu wasiruhisiwe kuvuka.Hata hivyo, agizo hilo lilisitiswa kufuatia hofu ya usalama na matatizo ya uchukuzi wa mizigo kivukoni hapo.

Waziri James Macharia alikuwa ametoa agizo kwa mkurugenzi wa Shirika la Huduma za Feri (KFS) Bakari Gowa kusitisha huduma kwa watumizi wa feri wanaotumia miguu.

Barua hiyo ya Machi 24 ilimtaka Bw Gowa kuagiza watu wanaovuka kwa miguu kupanda magari ili kuhakikisha kuwa kuna nafasi kati yao wanapovuka ili kuepuka kusambaza virusi vya xzorona.

Vile vile, barua hiyo ilieleza kuwa watu waruhusiwe kuvuka kwa kutumia matatu ambazo kwa kawaida huwa hazivuki kivuko hicho cha Likoni.Hata hivyo, jana kamishna wa Kaunti ya Mombasa Gilbert Kitiyo alisema kuwa agizo hilo limesitishwa.

“Agizo hilo limesitishwa kwa sasa. Watumizi wa feri wanaovuka kwa miguu wanaendelea kutumia feri hizo,” akasema Bw Kitiyo.Kulingana na wadokezi wa Taifa Leo, uamuzi huo wa kusitisha agizo hilo kutoka kwa wizara uliafikiwa baada ya washikadau wa kaunti ya Mombasa kukutana.

Mkutano huo ulihusisha maafisa wa kamati ya kupambana na corona Mombasa, Kamishna Kitiyo, Bw Gowa, maafisa wa uchukuzi wa kaunti na maafisa wa shirika la Msalaba Mwekundu.

“Jambo kuu lilikuwa hofu kuwa maelfu ya watu wanaotumia kivuko hicho wataleta rabsha iwapo watakongamana pamoja kivukoni hapo na kuambiwa kuwa hawaruhusiwi kuvuka,” akasema afisa mmoja wa kamati hiyo.

Katika mkutano huo, aidha suala la biashara pia lilizuka huku maswali yakiulizwa kuhusu wafanyabiashara wadogo wanaotumia kivuko hicho kuvukisha bidhaa zao.Ilikubadilika katika mkutano huo kuwa agizo hilo liwekwe kando na majadiliano zaidi yafanyike.

Baada ya mkutano huo ndipo Bw Kitiyo badala yake alitangaza kuwa watumizi wa feri watumie vifaa vya uso ambavyo vitawasaidia kusitisha kuambikizwa virusi vya COVID-19.

Vile vile Bw Kitiyo alisema kuwa watu ambao wanajihisi wapo na dalili za homa ya mafua wajitenge na watu.Aidha, kufikia jana ni watu wachache pekee walionekana kuwepo na vifaa hivyo.

Wengi, hata hivyo walikuwa wanaosha mikono kabla ya kuingia kwenye feri.

You can share this post!

Wakazi walia vibanda vya video vinawaharibia watoto

CORONA: Ruto kupokea mshahara wa chini zaidi

adminleo