Corona: Maduka ya Eastleigh yafungwa
Na CHARLES WASONGA
WAFANYABIASHARA wa Eastleigh, Nairobi wamefunga maduka makubwa katika mtaa huo ili kuzuia kusambaa kwa virusi vya corona.
Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyabiashara wa Maduka makubwa mtaani humo Omar Hussein alisema walichukua hatua hiyo baada ya kubaini kuwa watu katika majengo hayo ya kibiashara huwa hawazingatia masharti ya serikali ya kutotangamana.
“Maduka yote ya bidhaa mbalimbali yatafungwa kuanzia leo (Ijumaa) maduka yote yatafungwa kwa muda usiojulikana. Tumechukua hii bila notisi ili kuzuia watu kufurika zaidi kwenye maduka na kujiweka katika hatari ya kuambukizwa virusi hivyo,” Hussein akawaambia wanahabari Ijumaa.
Aliitaka serikali kuanzisha shughuli ya unyunyiziaji dawa katika barabara za mtaa huo pamoja na uzoaji taka wakati huu ambapo maduka hayo yatasalia kufungwa.
“Vile vile, tunaiomba Wizara ya Afya kuanzisha zoezi la kuwapima watu kwa wingi katika eneo hilo kwa sababu eneo hilo la kibiashara huvutia watu kutoka pembe zote za nchini,” Bw Hussein akaongeza.
Duru zasema kuwa mitaa ya Eastleigh na South C iko katika hatari ya kushuhudia maambukizi makubwa ya ugonjwa wa Covid-19 kwa sababu ina idadi kubwa ya watu na majengo makubwa ya kibiashara.
Mnamo Ijumaa Waziri wa Afya Mutahi Kagwe alitangaza kuwa wizara yake sasa iko tayari kuanzisha mpango wa kuwapima watu kwa wingi baada ya kupokea vifaa zaidi kutoka wahisani kutoka ng’ambo.
“Tutaendesha zoezi hilo kwa mpango; kuanzia mitaa ya mabanda yenye watu wengi hadi maeneo ambayo tumebaini kuwa katika hatari ya kushuhudia maambukizi zaidi,” akasema katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA), Nairobi alipokea rasmi shehena ya vifaa kutoka China.
Mitaa yote ya Nairobi imerekodi visa vya maambukizi ya virusi vya corona tangu Machi 13 kisa cha kwanza kiliporipotiwa nchini, kulingana na Waziri wa Afya Mutahi Kagwe.
Kwenye taarifa yake ya kila siku kuhusu janga hili, Waziri alisema Nairobi ina jumla ya visa 193 kati ya visa vyoye 262 ambavy vimethibitishwa nchini kufikia jana, baada visa 16 zaidi kuripotiwa jana.
Nairobi inafuatwa na kaunti ya Mombasa ambako kumeripotiwa visa 43. Kaunti za Kilifi na Kwale pia vimeripoti visa sita na 16, mtawalia.
“Ili kuchambua zaidi hali jijini Nairobi, mtaa wa Kilimani una visa sita, Kawangware (6), Karen (5), Utawala (4), Mlolongo (1) na Ngara (2),” akasema Kagwe.
Aliongeza kuwa mitaa ya Tassia, Buruburu, Parkalands, Buru Buru, na Kibera yote ina wagonjwa wawili wa Covid-19 kila moja.
Mitaa mingine jijini Nairobi kama vile Donholm, Eastleigh, Hurlingham, Lavington, Runda, Madaraka, na Kasarani pia imerekodi visa vya maambukizi.
Kaunti ya Mandera imerekodi visa vine, Nakuru (2), Siaya (2) huku Uasin Gishu, Kwale, Machakos, Homa Bay na Kakamega vimeripoti kisa kimoja kila moja.
Vile vile, Waziri Kagwe ameripoti kuwa wagonjwa wengine saba wamepona na kuruhusiwa kwenda nyumbani huku wawili zaidi wakifariki.
“Kwa hivyo, idadi jumla ya wale waliopona kufikia sasa ni 60 huku idadi ya walifariki ikitimu 12,” Bw Kagwe akawaambia wanahabari nje la makao makuu ya wizara yake, Jumba la Afya, Nairobi.