CORONA: Raia wamiminika madukani
Na PHYLLIS MUSASIA
MADUKA ya jumla mjini Nakuru yanaendelea kushuhudia msongamano wa wateja wanaomiminika kununua bidhaa mbalimbali kwa hofu ya virusi vya corona.
Bidhaa nyingi za nyumbani kama vile sukari, unga wa ugali, mafuta ya kupikia, dawa ya kuua viini mikononi, miongoni mwa bidhaa nyinginezo zimeonekana kupungua kwa kasi katika maduka hayo.
Wauzaji wanasema huenda kukawa na upungufu mwingi kufikia mwishoni mwa wiki hii ikiwa msongamano huo utaendelea.
Katika duka la Gilannis, foleni ndefu zilishuhudiwa huku wateja wakilazimika kusuburi kwa muda wa zaidi ya dakika 30 kabla ya kuhudumiwa.
Mhudumu mmoja wa duka hilo alisema msongamano huo ulianza mapema Ijumaa baada ya serikali kutangaza kisa cha kwanza cha ugonjwa huo humu nchini.
Alisema wahudumu wamelazimika kuongeza saa za kuhudumu ili kukabili idadi hiyo kubwa.
“Mara nyingi huwa tunashuhudia msongamano kama huu mwishoni mwa mwezi lakini sasa imekuwa tofauti na siku za hapo awali,” akasema.
Baadhi ya wahudumu walionekana katika sehemu ya lango kuu wakiwanyunyuzia wateja dawa hiyo ya kusafisha mikono kabla ya kuingia ndani.
Mapema Jumatatu, duka la Gilannis lilishuhudia upungufu wa matoroli ya kubebea bidhaa.
Waliofika kuchelewa, walilazimika kusubiri nje ili kuwapa muda wenzao waliokuwa ndani.
Wahudumu walisema msongamano huo umekuwa ukishuhudiwa kwanzia mapema asubuhi kila siku hadi jioni na hata kuwalazimu kuongeza muda fulani kabla ya wao kufunga kazi.
“Kazi ni nyingi hapa na idadi kubwa ya watu wanaingi na kutoka mara kwa mara. Sisi wenyewe tumeingiwa na uoga na hatuna uhakika ikiwa tutakuwa salama humu ndani,” akasema muhudumu mwingine ambaye alionekana kufanya kazi bila vifaa maalumu vya kumkinga na maambukizi ya corona.
Katika maduka la Tuskys, QuikMart na Naivas, hali ilikuwa vivyo hivyo.
Maduka hayo yaliripoti kukosa kemikali maalumu ya kusafisa mikono huku yakiwashauri wateja wanunue bidhaa kama vile sabuni za kawaida na zile za kuua viini kama chaguo mbadala.
Baadhi ya wakazi waliohojiwa walisema biashara zao zimeharibika na wengi wao hawana pesa za kutosha kununua vyakula vya kuwasaidia ikiwa serikali itatangaza marufuku ya kazi na sehemu nyinginezo.
Bw Festus Yego muuzaji wa nguo za mitumba alisema imekuwa vigumu kwake kupata wateja ikilinganishwa na siku za hapo nyuma.
Wafanyi biashara wengine kama vile wa kuuza vyakula walielezea wasiwasi wao huku wakisema wateja wao wamepungua kwa kiasi kikubwa na huenda siku za usoni wakawakosa kabisa kwani wengi wao huwa ni wanafunzi.