Habari MsetoSiasa

CORONA: Ruto kupokea mshahara wa chini zaidi

March 26th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na CHARLES WASONGA

RAIS Uhuru Kenyatta Jumatano aliongoza maafisa wakuu serikalini kupunguza mishahara yao, kama sehemu ya kusaidia serikali kupata pesa za kutosha kukabili maambukizi ya virusi vya corona.

Hii ina maana kuwa Rais Kenyatta atapokea Sh280,000 pekee kama mshahara badala ya Sh1,400,000 wa naibu wake akipata Sh240,000 badala ya Sh1,200,000.

Akihutbu jana katika Ikulu ya Nairobi, Rais alitangaza kuwa mawaziri na wasaidizi wao wamepunguziwa mshahara kwa asilimia 30 na 20 mtawalia.

Sasa mawaziri watapokea Sh646,800 badala yaSh 924,000 huku makatibu wakipata Sh612,000 kwa mwezi badala ya Sh765,000.

Katika orodha ya maafisa hao wote, Naibu Rais William Ruto ndiye atakuwa akipokea mshahara wa chini zaidi (Sh240,000) akifuatwa na Rais Kenyatta.

“Katika kugawanya mzigo huu unaotokana na hali ya sasa ya tishio la kiafya, kwa muda wote ambapo tutakuwa tunakabiliana nalo, kuanzia leo hii, utawala wangu umeamua kwa hiari kupunguza mishahara ya maafisa wakuu wa serikali,” akasema Rais.

Aliwahimiza wakuu wa idara nyingine za serikali kuiga mfano huo.