CORONA: Salamu za mikono zapigwa marufuku Mombasa
Na WINNIE ATIENO
KAUNTI ya Mombasa imepiga marufuku wakazi kusalimiana kwa mikono, kukumbatiana au kubusiana kama mojawapo ya mbinu za kujihadhari na maradhi hatari ya virusi vya corona.
Hatua hiyo imechukuliwa huku maafisa wa afya wakiendelea kukusanya orodha ya wageni wanaoingia nchini kupitia Bandari ya Mombasa.
Kufikia jana zaidi ya watu elfu mia moja walikuwa wameambukizwa ugonjwa huo duniani. Lakini hakuna kisa chochote ambacho kimetangazwa na serikali ya Kenya.
Afisa Mkuu wa Afya katika Kaunti ya Mombasa Aisha Abubakar, alisema ijapokuwa utamaduni wa Waswahili na wakazi wengi wa Pwani ni kusalimiana kwa mikono, sasa itabidi wajizoeshe kupungiana pekee.
“Ili kukabiliana na usambazaji wa virusi vya corona, inatupasa tuweke mikakati hii. Badala ya kuamkuana kwa kushikana mikono, heri tupungiane mikono. Najua kimila ni sharti tusalimiane lakini kutokana na tishio la ugonjwa huu, inatubidi tusitishe tabia hii ya kigeni kwa muda,” akasema Bi Abubakar.
Uamuzi huo unatokana na Mombasa kutajwa kati ya kaunti 14 zilizo kwenye hatari kubwa ya watu wake kuambukizwa virusi hivyo, ambavyo jana viliua mtu wa kwanza barani Afrika nchini Misri. Marehemu ni raia wa Ujerumani aliyekuwa amezuru Misri.
Bi Abubakar aliwasisitizia wakazi kuhusu umuhimu wa kuosha mikono kwa maji safi yanayonyunyuzika na sabuni na kutaja dalili kuu za ugonjwa huo kuwa na joto mwingi mwilini, matatizo ya kupumua na kukohoa.
“Ukikohoa au kuchemua tumia kitambaa ili kuzuia kuambukiza wengine. Ugonjwa huu unasambaa haraka sana,” akasema Bi Abubakar.
Mombasa, ambayo ni kitovu cha utalii nchini, ni lango la kuingilia Kenya kupitia baharini, angani na nchi kavu. Ina uwanja wa ndege wa kimataifa wa Moi na bandari ya Kilindini.
Kaunti nyingine ambazo zimetajwa kuwa zenye uwezekano wa kuwa kiingilio cha virusi hivyo ni Nairobi, Kisumu, Kiambu, Uasin Gishu, Kajiado, Busia, Migori, Kilifi, Kakamega, Kajiado, Nakuru, Wajir na Garissa.
Mbali na hatua za kupiga marufuku salamu, Kaunti ya Mombasa na zile za Kilifi na Garissa pia zinahamasisha wanafunzi na umma kwa jumla kuhusu njia za usafi unaowezesha kuepukana na ugonjwa huo.
Kaunti hizo pia zimetenga sehemu maalum za watu wanaoshukiwa kuambukizwa wanakoweza kutengwa wakifuatiliwa hali zao ama kutibiwa.
Waziri wa Afya wa Mombasa Hazel Koitaba, alisema wodi malaum ya watu wanaoshukiwa kuwa na ugonjwa huo imetengwa katika Hospitali Kuu ya Pwani.
Waziri wa Afya wa Garissa Dkt Ahmed Nadhir, alisema wameweka mipango ya kuzuia maambukizi, lakini wana wasiwasi iwapo yatatokea taifa jirani la Somalia.
“Pia tunawahamasisha wakazi dhidi ya ugonjwa huo siku tatu kwa wiki. Tulikuwa na mkutano na Waziri wa Afya Mutahi Kagwe na baraza la magavana kujadili suala hili. Tumeweka mikakati ya kukabiliana na dharura ya corona,” akasema.
Mwenzao wa Kilifi, Dkt Anisa Omar alisema wahudumu wa afya wanaendelea kushika doria katika uwanja wa ndege wa Malindi kuhakikisha wageni wote wanakaguliwa.
“Tumeunda jopo maalum linalosimamia dharura. Pia tumewapa mafunzo maafisa wa afya. Wanafunzi katika shule zote pia wanaendelea kupewa hamasisho ili waweze kuosha mikono kwa sabuni kila mara,” akasema.