• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 8:50 AM
CORONA: Wakazi Nakuru waumia

CORONA: Wakazi Nakuru waumia

NA RICHARD MAOSI

[email protected]

Mataifa yote ulimwenguni yameathirika na janga la Covid -19, huku ikiaminika kuwa zaidi ya theluthi mbili ya raia katika mataifa yanayoendelea watapoteza ajira kufikia mwisho wa Aprili endapo hali haitadhibitiwa.

Takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaonyesha kuwa zaidi ya watu 800,000 wameathirika, mataifa ya bara ulaya na Marekani yakipata pigo zaidi.

Ni kwa sababu hiyo unyanyapaa, kufunga mipaka ndani na nje na pia kuyakwepa mataifa yaliyoshuhudia maambukizi kumekuwa kikwazo cha maendeleo ya kiuchumi duniani..

Kufutiliwa kwa safari za ndege, sekta ya biashara, kufunga viwanda na kupunguza shughuli za utalii kumepunguza uwekezaji huku umaskini ukiendelea kukodolea macho bara la Afrika ambalo halina nyenzo za kujikinga.

Ingawa wizara ya Afya nchini Kenya inajaribu kuweka mikakati, juhudi zake hazionekani kuleta mabadiliko huku idadi ya watu walioambukizwa ikifikia 50 katika kipindi cha wiki mbili.

Katika maeneo ya kufanyia biashara, steji za basi, mikahawa, sehemu za umma za kupumzika na vituo vya kutoa huduma muhimu pamewekwa ndoo na sabuni za kusafisha mikono.

Aidha raia wamepatiwa ilani ya kutosalimiana kwa mikono pale wanapotangamana katika barabara huku maeneo yaliyokuwa yakishuhudia msongamano mkubwa wa watu siku za awali yakibaki kuwa tupu.

Kupungua kwa hazina ya chakula

Taifa Leo Dijitali iliwatembelea baadhi ya wafanyibiashara katika soko la Afraha Nakuru, kudadisi jinsi biashara zao zilikuwa zimeathirika tangu wahamishwe kutoka Top Market na Wakulima Market wiki iliyopita.

Tulikutana na Peter Muruka anayesimamia wachuuzi katika soko la Top Market akiendelea kupanga matunda na mboga kama kawaida yake, lakini hivi karibuni ameshuhudia uhaba mkubwa wa fedha.

Anasema kwa kipindi cha wiki moja tu mauzo yalikuwa yameshuka kutoka 3000 kwa siku hadi 300, hivi kutokana na uhaba wa wanunuzi wanaofika sokoni, hali inayosababisha kuwa na mfumko mkubwa wa bei ya bidhaa.

Baadhi ya matunda yalikuwa yameoza na alikuwa akitafuta mbinu ya kuyatupa, akitaja kuwa hii ni hasara kubwa kwani baadhi ya wakulima kutoka Dundori, Molo,Olenguruone na Bahati walikuwa wameacha kupeleka mazao yao sokoni.

Kulingana na Muruka anaona kuwa hazina ya chakula nchini ipo hatarini kwa sababu wakulima wengi hawana mipango ya kupanda msimu huu kwa sababu ya ukosefu wa soko kwa bidhaa zao, viwanda vya kutengeneza mbolea vilikuwa vimefunga.

“Wafanyibiashara wengi hapa wanalia hali ngumu ya uchumi kutokana na ukosefu wa wanunuzi na kusema ukweli pesa zimepotea,” akasema.

Anasema siku zilizopita kipindi kama hiki wanunuzi huwa wamefurika sokoni kutalii na kujipatia mahitaji yao ya kila siku lakini hali imebadilika, tangu janga la Corona litangazwe rasmi.

Aidha Muruka anasema kwa siku moja utakuta kuwa wateja wanaofika sokoni haizidi 200, kinyume na awali ambapo zaidi ya watu 1000 wangefika kufanya biashara.

Allan Songok 26 ni kijana anayefanya kazi ya kuwabebea wanunuzi mizigo hadi kwenye steji ya mabasi lakini sasa anategemea vibarua vya kuzoa takataka, kutoka kwa wauzaji wanaompatia 20.

Kulingana na Songok, tangu magari yahamishwe kutoka katikati ya jiji la Nakuru na kupelekwa katika eneo la Kingdom Seekers kilomita mbili hivi kutoka mjini, polisi wanaoshika doria wamekuwa wakiwahangaisha vijana wanaotegemea kazi ya kubeba mizigo.

Ukiukaji wa haki za kibinadamu

Swala la kuzingatia haki za kibinadamu bado ni changamoto nchini hasa wakati huu ambapo wakenya wanashuhudia kafyu ya kutotoka nje usiku, katika juhudi za kupigana na janga la Covid -19.

Hii ikiwa ni wiki ya kwanza tayari watu wengi wameharibiwa mali yao na polisi wanaotumia nguvu kupita kiasi, na kuwajeruhi hata wale wasiokuwa na hatia katika makazi yao.

Zakayo Rutto mkaazi wa Top Ten Nakuru ni muuzaji wa maziwa ambaye anafanya kazi ya kusambaza maziwa kwa wakazi wa mitaa ya Nakuru kama vile Rhonda na Kaptembwa.

Anasema tangu rais Kenyatta atangaze kafyu watu wote walitii na yeye amekuwa akifunga kazi yake 6.00 jioni, ili kujiepusha na askari wanaoshika doria kuhakikisha raia wanatii amri.

Siku ya Jumamosi Rutto alivamiwa na polisi 8.00 usiku akiendelea kuchemsha maziwa yake lita 40.Alieleza kuwa vurugu ilizuka pale alipokataa kuwafungulia mlango usiku kwa kuacha dirisha wazi.

Rutto anasema aliacha dirisha wazi baada ya kufunga duka ili hewa safi iweze kuingia, lakini polisi wakashikilia kwamba alikuwa akiendelea na biashara wakati huo.

Kulingana naye alipokataa kuwafungulia walitumia rungu zao kuvunja vioo vya dirisha ambapo baadhi yazo zilitapakaa ndani ya maziwa na kumsababishia hasara., ya siku hiyo ikizingatiwa hakuwa na kazi nyingine ya kufanya.

“Ningependa kueleza inspekta wa polisi Bw Mutyambai kuwa anaongoza genge la wahalifu na wala sio walinda usalama,” akasema.

Hatimaye polisi walitoroka pale majirani walipofungua milango yao ili kuokoa jamaa.

Anasema kuwa janga la Corona limekuja kuharibu mali ya watu, na hadi wakati wa mahojiano haya Rutto alikuwa ameripoti kisa hiki Bondeni Police post na Flamingo.

Anasema yeye amekuwa akifanya kazi ya kutafuta maziwa hadi katika maeneo ya Bahati Nakuru, ili aweze kumudu mahitaji ya familia yake.

Anasema gharama ya kukarabati vioo ni ghali sana hasa wakati huu ambapo pesa zimeadimika na anatumai kuwa kamishna wa Bonde la Ufa Bw George Natembeya atachukua hatua dhidi ya walinda usalama hao, huku tayari uchunguzi ukiwa umeanzishwa.

Ukosefu wa huduma muhimu za mahakama kutetea haki

Ni kwa sababu hiyo muungano wa mawakili kutoka Bonde la ufa siku ya Jumamosi waliomba jaji mkuu David Maraga kurejelea vikao kwa korti ili kuhakikisha wakenya wanalindwa dhidi ya dhulma za polisi.

John Ochang rais wa mawakili kutoka Bonde la Ufa akiomba jaji mkuu kufungua huduma za mahakama ili kuwakabili polisi wanaowahangaisha raia. Picha/ Rcihard Maosi

Wakiongozwa na John Ochang rais wa mawakili kutoka Bonde la Ufa alisema , polisi wanafaa kudhibitiwa ili kuendesha shughuli zao ipasavyo ili kutekeleza marufuku ya kutoka nje usiku.

Aidha anaomba serikali iwachukulie polisi walioonekana kwenye kanda za video hatua kali, kwa kutekeleza unyama dhidi ya raia, kwani alikuwa akiunga mkono marufuku ya kutotoka nje usiku lakini aliomba itekelezwe kwa njia inayofaa.

“Bila kufanya hivyo basi huenda umma ikapoteza imani na vyombo vya usalama ambavyo vinastahili kuwalinda dhidi ya hatari,” akasema.

Anaona kuwa polisi walikuwa wamesahau majukumu yao, kuhakikisha kuwa sheria zilikuwa zikifuatwa na hivi sasa wameanza kutekeleza majukumu ya mahakama.

Aidha anasema vikao vya mahakama vitazingatia kanuni ya mshtaki na mstakiwa kukaa upande kwa mita moja ili kupunguza hatari ya kuambukizwa virusi vya Corona.

You can share this post!

Afueni kwa wafanyabiashara baada ya soko kufunguliwa

Joho atuza mama aliyejifunika chupa kuzuia corona

adminleo