Habari Mseto

CORONA: Wakazi waonywa dhidi ya kula sahani moja

March 26th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na WAWERU WAIRIMU

SPIKA wa Bunge la Kaunti ya Isiolo Hussein Roba amewarai wakazi wakomeshe utamaduni wa kula kwenye sahani moja, wakati huu maambukizi ya virusi vya corona yanaendelea kutikisa nchi.

Wakazi wa jamii za kuhamahama na Waislamu huwa na tabia ya kula kutoka kwa sahani moja, itikadi ambayo inaweza kuwaweka kwenye hatari ya kuambukizwa virusi vya corona.

‘Ninawaomba wakazi hasa Waislamu kujizuia kula kwenye sahani moja hadi hivi virusi vituondokee,’ akasema Bw Roba.

Miongoni mwa jamii nyingi za Waislamu, kawaida chakula huwekwa kwenye sahani moja kubwa na kila mtu akamega kutoka upande wake.

Spika huyo pia aliamrisha kwamba sehemu ya Sh40 million ambazo zilipitishwa na bunge la kaunti ili zitumike kupigana na ueneaji wa corona, zitumike kuwafidia wafanyabiashara ambao wanaendelea kupata hasara kutokana na janga hilo.

Alisema serikali ya Gavana Mohammed Kuti inafaa kushirikiana na machifu na manaibu wao katika kutambua wafanyabiashara ambao wameathirika zaidi ili wapewe msaada wa kifedha.

‘Tutunzane na kujali maslahi ya majirani wetu. Tusihodhi vyakula ilhali wenzetu ambao mapato yao yameathirika wanalala njaa,’ akaongeza.

Pia aliwataka wazazi wawe waangalifu na kuwazuia watoto wao kurandaranda maeneo tofauti kama tahadhari ya kuwazuia wapate virusi vya corona.

Aliwahimiza wakazi kuheshimu na kuzingatia mikakati iliyotolewa na Wizara ya Afya kama vile kunawa mikono na kuzingatia kiwango vya juu vya usafi nyumbani na maeneo ya umma.