CORONA: Wataalamu waonya Wakenya dhidi ya matumizi holela ya dawa
Na MAGDALENE WANJA
SHIRIKA la Wanafamasia Nchini (PSK) limewaonya Wakenya dhidi ya kujitibu au kununua dawa zozote za kutibu maradhi ya Covid-19 yanayosababishwa na virusi vya corona.
PSK imetoa tangazo hilo kufuatia kusambaa kwa habari ambazo hazijabainishwa kwamba kuna baadhi ya dawa ambazo zimethibitishwa kutibu virusi vya corona, baadhi ya watu wamekuwa wakinunua dawa hizo madukani bila ushauri wa daktari.
Baadhi ya dawa zilizotajwa ni pamoja na chloroquine, hydroxy chloroquine, azithromycin na zile zinajulikana kama antiviral medicine.
“Tabia kama hizi ni hatari sana hasa ikizingatiwa kuwa ugonjwa huu unaweza kuwa mojawapo ya changamoto kuu katika afya ya binadamu,” imesema PSK kwenye taarifa.
PSK imeongeza kuwa watu wanaonunua dawa hizi kwa viwango vikubwa wanahatarisha maisha ya wagonjwa wenye maradhi mbalimbali ambao huzitegemea dawa hizi kwa maisha yao ya kila siku.
PSK pia imeonya kuwa ununuzi wa dawa hizo bila ushauri wa mtaalamu wa maswala ya afya ni kinyume cha sheria na unaweza ukasababisha kutozwa faini kubwa au kuhudumu kifungo cha gerezani.