• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 8:50 AM
CORONA: Waziri asema ada ya kupimwa ni Sh1,000

CORONA: Waziri asema ada ya kupimwa ni Sh1,000

Na CECIL ODONGO

WANAOPIMWA virusi vya corona katika hospitali za umma wanapaswa kutozwa Sh1,000 pekee, Waziri wa Afya Mutahi Kagwe alisema Jumatatu.

Hii ni kinyume na hali ambapo hospitali za umma ikiwemo Kenyatta (KNH) inatoza Sh5,000 kwa wanaopimwa virusi hivyo.

Nazo hospitali za kibinafsi zinatoza Sh8,000 kwenda juu.

Waziri Kagwe alisema wanaopimwa kwenye shughuli za umma hawatozwi pesa zozote.

“Kuna wale ambao wangependa kupimwa kwenye maabara ya kibinafsi na hospitali za serikali. Katika hospitali za serikali, watapimwa kisha watozwe Sh1,000. Tunaendelea kuwapima wagonjwa wa Covid-19 pekee katika hospitali ya Mbagathi,” akasema.

Waziri alitangaza kuwa wagonjwa 65 zaidi wameruhusiwa kuondoka hospitalini na kufikisha idadi ya waliopona hadi 2,946.

Nayo idadi ya waliokufa ilipanda hadi 197 baada ya watu wengine 12 kufariki kutokana na virusi vya corona kulingana na takwimu alizotangaza waziri.

Bw Kagwe pia alitangaza visa vipya 189 na kufikisha idadi ya waliopata virusi hivyo tangu Machi kuwa watu 10,294

Hii ni baada ya sampuli 1,205 kupimwa kwa muda wa saa 24 zilizopita.

Bw Kagwe aliwataka Wakenya wafuate maagizo yaliyotolewa ili kuzuia maambukizi mapya hasa baada ya serikali kuondoa marufuku ya usafiri katika Kaunti za Nairobi, Mombasa na Mandera wiki iliyopita.

Pumwani

Pia alifichua kuwa wahudumu 22 wa afya katika hospitali ya Pumwani, Nairobi walipatikana na virusi hivyo.

baada ya shughuli ya kupima umma kuendeshwa hospitalini humo.

Alikariri kwamba hakuna malipo yanayotozwa kwenye vipimo vya umma na akawashauri watu wakumbatie shughuli hiyo ili kufahamu iwapo wana Covid-19 au la.

Alitangaza kuwa kaunti 13 zitapata magari ambayo yameigharimu serikali Sh200 milioni ili zitumike kuwafuatilia watu waliotangamana na wenye virusi vya corona.

“Tuna kikosi cha watu 229 katika kaunti zote ambao wanafuatilia wale waliotangamana na waliopatikana na virusi vya corona. Tumewapa mafunzo ya kutumia teknolojia,” akaongeza.

You can share this post!

Mama, mtoto wafungiwa na ajenti kwa kushindwa kulipa kodi

EPL: Obafemi ainyima Manchester United fursa ya kuingia...

adminleo