Habari Mseto

CorpAfrica na KSG zazindua mipango ya kuhakikisha vijana wanakumbatia ubunifu

Na HAPPINESS LOLPISA April 11th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

SHIRIKA la CorpsAfrica limeanza ushirikiano na Taasisi ya Mafunzo kuhusu Utawala (KSG) kutoa mafunzo kuhusu ujasiriamali na ubunifu miongoni mwa vijana.

Akiongea wakati wa uzinduzi wa mpango huo, Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo Dkt Patricia King’ori-Mugendi alisema suluhu kwa changamoto zinazowasibu vijana haziwezi kushughulikiwa kwa wao kuhamia mijini bali kujitegemea kwa kuanzisha biashara za kujiletea mapato.

“Kuhamia miji kutawaleta vijana mahangaiko zaidi. Hii ni kwa sababu kuna mengi ambayo vijana wanaweza kufanya kujiletea mapato badala ya kuhangaika mijini,” akasema Dkt Mugendi. 

Wakati huu, shirika la CorpsAfrica linaendesha shughuli zake katika nchi 10 za Afrika ambako limeanza miradi itakayowawezesha vijana kati ya umri wa kati ya miaka 20 na 27 kujiongezea ujuzi wa kuwawezesha kujiendeleza siku za usoni.

Shirika hilo limekuwa likitambua miradi ambayo inanufaisha jamii kisha kuifadhili kwa angalau asilimia 25. Miradi hiyo japo huwa ni midogo huwa inaathari chanya tena  ya moja kwa moja katika jamii.

Mpango huu unatofautiana na ule ambao umezoeleka ambapo jamii huwa inatagemea miradi yao yote ifadhiliwe na mashirika yasiyo ya kiserikali na hutegemea mashirika hayo kabisa kiasi kuwa yakiporomoka yanasalia mahame.

Kwa mujibu wa Dkt Mugendi, wanatoa mafunzo kwa vijana na hata kusaidia kuwasafirisha wengine ngámbo kwa mafunzo ya kazi ili wawe wakijitegemea.

“Hapo wanapata uzoefu wa majukumu mbalimbali kisha wanapata pia ujuzi ambao pengine hawawezi kupata kupitia mafunzo darasani,” akaongeza.