COVID-19: Himizo watu wale chakula chenye virutubisho vya kutosha
Na SAMMY WAWERU
CHAKULA chenye madini na virutubisho vya kutosha kinasaidia kupunguza makali ya ugonjwa wa Covid-19.
Wizara ya Afya imeshauri watu kukumbatia ulaji wa mlo wenye virutubisho, ikisema unasaidia kwa kiasi kikuu katika vita dhidi ya janga la corona.
Waziri Msaidizi katika Wizara, Dkt Rashid Aman amesema Ijumaa kwamba mbali na kuimarisha kinga ya mwili, vyakula vyenye virutubisho vya kutosha na madini kamilifu, vinapunguza hatari inayojiri kupitia ugonjwa wa Covid-19.
Akizungumza wakati akitoa taarifa ya corona Afya House, Nairobi, Dkt Aman pia amesema ulaji wa mlo wenye virutubisho unapunguza gharama ya matibabu kwa walioambukizwa.
“Kimsingi, ni muhimu watu wale chakula chenye madini faafu na virutubisho vya kutosha ili kukabili makali ya ugonjwa huu,” akashauri Dkt Aman katika kikao hicho na wanahabari na ambacho kwa mara ya kwanza tangu Kenya ithibitishe kisa cha kwanza cha Covid-19, waandishi hawakuuliza maswali.
Amesema walio katika hatari ya kuhangaishwa na corona ni wanaokula mlo duni, wenye matatizo ya maradhi sugu, kina mama wajawazito na pia watoto waliougua ugonjwa wa selimundu (Anemia).
Dkt Aman amedokeza kuwa takriban asilimia 25 ya idadi jumla ya Wakenya, wana matatizo ya upungufu wa damu mwilini.
Aidha, Dkt Aman amesema lishe duni kwa watoto hutatiza ukuaji wao.
Chini ya saa 24 zilizopita, Kenya imethibitisha visa vipya 241 vya Covid-19. Idadi hiyo inafikisha jumla ya maambukizi 33,630 yaliyoandikishwa nchini, tangu kisa cha kwanza kiripotiwe mnamo Machi 13, 2020.
Imekuwa habari njema kwa taifa, kwani chini ya 24 zilizopita hakuna kisa chochote cha kifo kutokana na Covid-19 kilichoripotiwa. Idadi ya walioangamizwa na ugonjwa huo imesalia 567.