COVID-19: Mbunge kudhamini wasanii wenye kazi za hamasisho
SAMUEL OWINO na CHARLES WASONGA
MBUNGE wa Saboti Caleb Amisi ameahidi kugharimia utayarishaji wa muziki utakaotungwa na Mkenya yeyote kwa lengo ya kuwafunza wananchi kuhusu kero ya virusi vya corona na vilevile kutoa hamasisho.
“Endapo kuna Mkenya ambaye atatunga wimbo mzuri wa kutoa uhamasisho kuhusu mbinu bora za kupambana na mkurupuko wa ugonjwa huu hatari ajitokeze. Nitabeba gharama yote ya utayarishaji wa wimbo huo,” akasema Bw Amisi katika taarifa.
Akaongeza: “Kuanzia muziki hadi sanaa, wimbo hadi ushairi na kutoka fasihi hadi drama, sharti tuibue nguvu na talanta zitakazotusaidia kuzima ugonjwa huu hatari.”
Mbunge huyo alisema alichukua aumuzi huo baada ya kung’amua kuwa wengi wa Wakenya haswa vijina, hawazingatii masharti yaliyotangazwa na serikali ya kuzuia maambukizi ya virusi hivyo.
Mnamo Alhamisi Waziri wa Afya Mutahi Kagwe pia alilalamika kuwa baadhi ya Wakenya hawachukulii kwa uzito mikakati iliyotangazwa na serikali ya kudhibiti kuenea kwa virusi hivyo.
Kwenye kikao na wanahabari, Bw Kagwe alisema kuwa watu wangali wanajikusanya katika maeneo ya umma kama vile mabaa na vilabu vya burudani katika vituo vya magari ya uchukuzi.
“Wakenya wanafaa kutambua kuwa virusi hivi ni hatari sio tu katika mataifa ya China na Italia bali hata humu nchini. Wakati mwingine tunashangaa kuwa baadhi ya wananchi hawachukulii janga hili kwa uzito,” Bw Kagwe akasema.
Baadhi ya masharti ambayo serikali ilitangaza ni watu kutengana kwa umbali kwa mita moja u nusu, watu kutosalimiana kwa mikono na kuhakikisha wameosha mikono na kudumisha usafi kila mikono.
Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) linapendekeza uzingatiaji wa masharti kama haya katika sehemu za hatua za kuzuia kuenea kwa virusi vya corona.