COVID-19: Miongoni mwa visa vipya 105 kuna Wakenya 96 na raia wa kigeni 9
Na SAMMY WAWERU
WAZIRI Msaidizi katika Wizara ya Afya Dkt Rashid Aman ametangaza Jumatano kuwa wagonjwa 176 imethibitishwa wamepona Covid-19 na kuruhusiwa kuondoka hospitalini katika kipindi cha saa 24 zilizopita, hii ikiwa ni habari nzuri tangu Machi 13, 2020, kisa cha kwanza kiliporipotiwa.
“Leo tumeruhusu kuondoka hospitalini idadi ya juu zaidi ya wagonjwa waliopona ambao ni 176. Idadi hii inafikisha jumla ya 1,048 ya wagonjwa waliopona Covid-19 nchini,” amesema Dkt Aman.
Katika kipindi cha saa 24 zilizopita, maambukizi mapya 105 yamethibitishwa kutoka kwa sampuli 2,273 zilizokusanywa, kukaguliwa na kufanyiwa vipimo, idadi jumla ya maambukizi ya virusi vya corona nchini ikigonga 3,094.
Wakati huohuo, mgonjwa mmoja kutoka Nairobi ametangazwa kufariki kutokana na Covid-19, idadi ya wagonjwa waliofariki nchini kutokana na ugonjwa huu ambao sasa ni janga la kimataifa ikifika 89.
Maambukizi miongoni mwa madereva wa malori ya masafa marefu yameendelea kurekodiwa.
Katika visa vipya vya Jumatano, kaunti ya Busia imesajili maambukizi 18 ya madereva wa masafa, Turkana (7), Taita Taveta (3), Kisumu (2) na Uasin Gishu dereva mmoja.
“Suala la maambukizi ya virusi vya corona miongoni mwa madereva wa masafa marefu, hasa katika boda ya Kenya na Uganda, mpaka wa Busia na Malaba, tunalitilia maanani. Wizara ya Afya inashirikiana kwa karibu na serikali ya kaunti ya Busia kuliangazia,” Dkt Aman akaambia wanahabari katika kikao cha kila siku kueleza hali ya Covid-19 nchini, Afya House, Nairobi.
Waziri huyo alisema madereva wa mataifa ya kigeni wanaopatikana na corona hawaruhusiwi kuingia nchini. Alisema, madereva wa Kenya wanaopatikana na Covid-19 wanatengwa mara moja na kuanza kupata matibabu.
Ili kuruhusiwa kuingia Kenya au mataifa ya kigeni, madereva sharti wawe na cheti cha vipimo vya Covid-19 kinachodumu muda wa wiki mbili.