• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 5:50 AM
COVID-19: Mwanamke asiyeonyesha dalili awaambukiza watano Dandora

COVID-19: Mwanamke asiyeonyesha dalili awaambukiza watano Dandora

Na CHARLES WASONGA

VISA vipya vya maambukizi ya virusi vya corona vinaendelea kugunduliwa katika mitaa yenye watu wengi katika miji ya Nairobi na Mombasa.

Mtaa wa Dandora, Nairobi ni wa hivi punde kugonga vichwa vya habari baada ya kuandikisha visa vitano vya corona.

Kulingana na taarifa ya Wizara ya Afya iliyotolewa wa Waziri Msaidizi Rashid Aman Ijumaa jioni, watano hao ni miongoni kwa wagonjwa 16 wapya wa Covid-19 waliothibitishwa nchini hivyo kufikisha idadi jumla nchini kuwa 336.

Duru zinasema kuwa mwanamke mmoja katika mtaa wa Dandora Phase 4, ambaye hakuonyesha dalili za ugonjwa huo ndiye aliwaambukiza watu hao watano.

Watu wengine wanne ambao inasemekana kuwa alitangamana nao bado wanasakwa.

Mama huyo aligunduliwa kuwa na virusi vya corona alipoenda kufanyiwa uchunguzi wa kiafya, kutokana na ugonjwa mwingine ambao umemwathiri kwa muda mrefu, katika hospitali moja ya mmiliki binafsi mtaani humo.

Kando na Dandora visa vingine viwili viligunduliwa katika mitaa ya City Park, Parklands (2), Pangani (1) na Eastleigh (1).

Visa saba vipya viligunduliwa katika Kaunti ya Mombasa katika mitaa ifuatayo; Kiembeni (1), Centi Kumi (1), Stadium (1), Msikiti Nuru (1) na Mulaloni (1).

Watu hao 16 walipatikana kuwa na virusi vya corona baada ya sampuli 946 kufanyiwa uchunguzi.

Wakati huo huo, wagonjwa wengine watano wameruhusiwa kwenda nyumbani baada ya kupona, hivyo kufikisha idadi ya waliopona kufikia sasa kuwa 95.

Idadi ya waliofariki bado ilisalia kuwa 14, kufikia Ijumaa.

You can share this post!

Chelsea yahemea huduma za Aubameyang wa Arsenal

Seneti kuchunguza kifo cha Walibora

adminleo