COVID-19: Serikali yawataka raia wawe makini wasipotoshwe
Na SAMMY WAWERU
KUNA maelezo ya kupotosha kuhusu kinachotajwa ni matibabu ya Covid-19 yanayosambaa kwenye mitandao ya kijamii na pia kusambazwa na baadhi ya vyombo vya habari, serikali imeonya.
Wizara ya Afya imetahadharisha umma, ikitaka watu wafahamu kwamba corona haina tiba ila maambukizi yake yanadhibitiwa kwa kuzingatia kanuni na mikakati iliyowekwa.
Waziri Msaidizi katika Wizara Dkt Mercy Mwangangi amezitaka asasi za kupasha habari kuwajibika katika kinachosambazwa.
“Tunahimiza vyombo vya habari na asasi zingine husika kupasha umma taarifa zifaazo na kwa mujibu wa idara ya afya,” Dkt Mwangangi akasema akiwa Afya House, Nairobi, Ijumaa wakati akitoa takwimu za maambukizi ya corona nchini katika kipindi cha saa 24 zilizopita.
Waziri huyo amesema imebainika hasa kwenye mitandao ya kijamii, baadhi ya wachangiaji wanasambaza habari za tiba ya corona, alizotaja kuwa ni potovu kwa umma.
“Tumeona taarifa ya michanginyiko ya dawa, watu wakidai inaponya corona. Upashaji wa jumbe kama hizo unalemaza vita dhidi ya ugonjwa huu,” Dkt Mwangangi akaonya, akisema Wizara ya Afya imejikakamua kufanya matangazo ya habari zifaazo.
Ugonjwa wa Covid-19 haujapata chanjo wala tiba iliyoidhinishwa rasmi na Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) kufikia sasa, japo walioambukizwa wakizingatia ushauri na matibabu ya madaktari wanapona.
Madaktari, wataalamu wa masuala ya afya na matibabu, pamoja na Wanasayansi kote ulimwenguni wako mbioni kutafuta chanjo na tiba ya corona.
Ijumaa, katika kikao cha 147 kueleza hali ya Covid-19 nchini, Wizara ya Afya imetangaza maambukizi mapya 580, idadi hiyo ikifikisha jumla ya visa 29, 334 vya waliothibitishwa kuugua ugonjwa huo.
Wagonjwa 198 kutoka vituo mbalimbali vya afya na pia matunzo ya nyumbani wamethibitishwa kupona, idadi jumla ya waliopona nchini ikigonga 15,298.
Hata hivyo, katika kipindi cha saa 24 zilizopita Covid-19 imesababisha vifo vya watu watano, jumla ya waliothibitishwa kufariki kutokana na ugonjwa huu ikifika 465.