COVID-19: Upimaji wa watu wengi waanza Nakuru
Na PHYLLIS MUSASIA
KAUNTI ya Nakuru imezindua mpango wa kuchukua sampuli za watu wengi na kuzifanyia vipimo kujua ikiwa wana ugonjwa wa Covid-19 au la.
Mpango huo unalenga kuwafikia wafanyabiashara katika masoko mbalimbali, wamiliki na wahudumu katika hoteli miongoni mwa makundi tofauti ya watu katika kaunti.
Kulingana na Gavana Lee Kinyanjui, hatua hiyo itasaidia kuhakikisha maeneo ya biashara yako salama.
Aidha, mpango huo utasaidia kaunti kutekeleza kanuni zote zilizowekwa na Wizara ya Afya kwa biashara za hoteli na maeneo ya burudani.
“Idara ya afya ya umma inalenga kupima zaidi ya watu 10,000 katika sekta ya hoteli na biashara kwa muda wa wiki mbili zijazo,” akasema gavana Kinyanjui.
Afisa mkuu wa afya ya umma Dkt Samuel King’ori alisema shughuli hiyo itafanyika kila siku katika hospitali ya Nakuru tawi la Annex.
Afisa wa afya ya umma wa kaunti Dkt George Gachomba alisema jumla ya watu 600 wamepimwa tangu Jumatatu ambapo walithibitishwa kuwa salama.
“Shughuli hii inalenga sekta zote ambazo zimeangaziwa kuwa maeneo hatari kwa maambukizi ya virusi vya corona. Wafanyakazi wote wa sehemu za biashara ambazo zimeidhinishwa na idara ya afya ya umma watapewa kipaumbele,” akasema Dkt Gachomba.
Alisema sehemu za biashara 200 pekee katika kaunti nzima ndizo zimeruhusiwa kuendelea na shughuli na akatoa tahadhari kwa wale ambao wananuia kufungua biashara bila idhini kutoka kwa idara hiyo kwamba wataadhibiwa kulingana na sheria.
“Wafanyabiashara walioruhusiwa kuendelea na kazi watafanya hivyo chini ya kanuni zilizowekwa na pia kuhakikisha kuwa wako na vyeti maalumu vya siku 14 na matokeo ya vipimo vyao kila baada ya wiki mbili,” akaonya Dkt Gachomba.