Habari Mseto

COVID-19: Visa vipya 390

December 19th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na CHARLES WASONGA

KENYA Jumamosi iliendelea kuandikisha kushuka kwa kiwango cha maambukizi ya Covid-19 na idadi ya wagonjwa wanaofariki kutokana na homa hiyo hatari.

Kwenye taarifa kwa vyombo vya habari, Waziri wa Afya Mutahi Kagwe alisema kuwa ni visa 390 vipya vya maambukizi ya Covid-19 vilinakiliwa kote nchini baada ya sampuli kutoka kwa watu 6,277 kupimwa.

Idadi hiyo mpya imefikisha 94,151 idadi jumla ya maambukizi nchini tangu kisa cha kwanza kiripotiwe mnamo Machi 13. Idadi ya sampuli ambazo zimepimwa kufikia Jumamosi ni 1,003,493.

Vifo vya wagonjwa wanne zaidi vimefikisha 1,633 idadi jumla ya wagonjwa ambao wameangamizwa na ugonjwa huo.

Bw Kagwe pia alisema kuwa wagonjwa 52 wamelazwa katika vyumba vya kuwahudumia wagonjwa mahututi (ICU) ilhali wengine 25 wanaongezwa oksijeni ya ziada.

Idadi ya wagonjwa ambao wamelazwa katika wadi maalum za kawaida ni 844 ilhali wagonjwa 5,916 wanahudumiwa nyumbani, kulingana na taarifa hiyo.

“Kwa bahati nzuri jumla ya wagonjwa 285 wamepona na kuruhusiwa kurejelea maisha yao ya kawaida. Wagonjwa 241 walikuwa wakiuguzwa chini ya mpango wa uuguzi nyumbani ilhali wagonjwa 43 walikuwa wamelazwa katika hospitali mbalimbali,” akasema waziri Kagwe.

Kufikia Jumamosi idadi jumla ya wagonjwa ambao walikuwa wamepona tangu Machi 2019 ni 75,559.

Takwimu kuhusu maambukizi 390 mapya yamesambazwa katika kaunti mbalimbali nchini huku Nairobi ikiongoza kwa kunakili visa vipya 103.

Inafuatwa na Mombasa iliyoandikisha visa 50, Nakuru visa 48, Kitui (27), Embu (20), Kilifi (15), Migori (13), Uasin Gishu (12), Laikipia (12), Murang’a (11), Kiambu (10), Meru (9), Kakamega (8) na Baringo (6).

Busia, Nandi, Machakos , Garissa zina visa nne (4) kila moja, Kisumu na Trans Nzoia zina visa vitatu (3) kila moja, Siaya, Makueni na Turkana zina visa viwili (2) kila moja huku Taita Taveta, Kisii, Kirinyaga, Nyeri, Bungoma, Homa Bay, Vihiga na Kajiado zikinakili kisa kimoja kila moja.