• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 6:07 PM
COVID-19: Watoto Changamwe na Likoni watakiwa waache kuzurura

COVID-19: Watoto Changamwe na Likoni watakiwa waache kuzurura

Na MISHI GONGO

WASHIKADAU katika sekta ya watoto wamehimiza wazazi katika maeneobunge ya Changamwe na Likoni mjini Mombasa kuwazuia watoto wao kurandaranda.

Maeneobunge ya Changamwe na Likoni yametajwa kuongoza yakiwa na idadi kubwa ya watoto walioachiliwa kuzurura mitaani licha ya kuenea kwa ugonjwa wa Covid-19 mjini humo.

Washikadau hao walionya kwamba kuna uwezekano mkubwa wa watoto wengi kupata maambukizi ya ugonjwa huo hatari iwapo wazazi hawatawazuia watoto wao.

Mwezi Juni afisa mkuu wa afya katika mji huo Dkt Khadija Shikely alitoa tahadhari ya kutaka watoto wasiruhusiwe kuzurura baada ya watoto watatu walio kati ya umri wa miaka mitatu na tisa kupatikana na virusi vya corona.

Mwanachama katika mtandao wa haki za watoto Bi Agnes Mailu alisema tangu shule kufungwa watoto wengi wanaonekana wakirandaranda mitaani kutafuta ajira huku wengine wakicheza kiholela.

“Tunasikitika kuona watoto majaani wakiokota chupa na vyuma kwa ajili ya kuuza nao wengine wakitafuta kazi za nyumbani bila kujua hatari iliyopo kwao,” akasema.

Mwingine Bi Sofia Abdallah anayeshughulikia haki za watoto alisema ni wajibu wa wazazi kukaza kamba ili kuwaepusha watoto wao na maambukizi.

Wiki iliyopita Kamanda wa polisi eneobunge la Changamwe Bw Joseph Kavoo aliwaonya wanaoajiri watoto kufanya kazi za nyumbani.

Alisema tangu kufungwa kwa shule ili kudhibiti virusi vya corona, baadhi ya watoto wameanza kusaka ajira majumbani.

“Tunataka kutoa onyo, tutakapo kupata umemuajiri mtoto tutakuchukulia hatua za kisheria,” akasema.

Alieleza kuwa miongoni mwa kazi ambazo watoto hao wanazifanya ni kufua, kusafisha nyumba na kuokota vyuma vikuukuu na chupa kisha wakiviuza kujipatia mapeni.

“Serikali ili tangaza kufungwa kwa shule ili kuwalinda watoto.Wazazi kuruhusu watoto kuranda randa majumbani mwa watu kutafuta ajira ni kuhatarisha maisha ya watoto hao,” akasema Bw Kavoo.

Aidha aliwaonya wazazi ambao watoto wao watapatikana wakirandaranda au kujihusisha na ajira.

“Kila mzazi ahakikishe mtoto wake anajihusisha na kudurusu masomo yake na kusaidia nyumbani kwao wala si kuingilia ajira,” akasema.

Alisema watoto kuzuru nyumba tofauti kusaka ajira kunawaweka katika hatari ya kuambukizwa ugonjwa wa Covid-19.

“Kama ilivyotangaza Wizara ya Afya, watoto wako katika hatari kubwa ya maambukizi. Nyumba wanazoenda kufanya kazi huenda huko kukawa na mtu anayeugua virusi hivyo,” akasema

You can share this post!

Vimada wafyonza jasho la paparazzi

Baadhi ya Wajomvu waandamana Mombasa malalamiko yakiwa...

adminleo