Dai chokoraa walitelekezwa na kaunti lachunguzwa na seneti
Na ERIC MATARA
MZOZO uliozuka baada ya serikali ya Kaunti ya Nakuru kuwatelekeza watoto wa kurandaranda mitaani waliowasafirisha na kuwatupwa eneo la Torongo, Kaunti ya Baringo mapema mwaka huu, umefikia bunge la seneti.
Kamati ya bunge hilo kuhusu Leba imeanza kuchunguza suala hilo baada ya kikundi cha wakazi wa Nakuru kuiandikia barua iliyowasilishwa na Seneta Susan Kihika (pichani).
Wakazi wanataka serikali ya kaunti hiyo kuadhibiwa kwa kufanya hivyo, na pia sheria zitungwe kuwalinda watoto wa mitaani kutokana na dhuluma.
“Tunaomba seneti kuchunguza kisa hiki na kuhakikisha kuwa familia za mitaani zinaheshimiwa na kukingwa kutokana na kuvunjiwa haki,” sehemu ya barua hiyo ilisema.
Kamati hiyo sasa ina siku 60 kushughulikia maombi ya wakazi, kabla ya kuwasilisha ripoti mbele ya bunge.
Seneta Susan Kihika alitaja hatua ya serikali ya Gavana Lee Kinyanjui kuwa ya kuchukiza na iliyokiuka haki za binadamu na za kikatiba za familia za mitaani.
“Hatua hiyo haikuwa ya utu na haifai kufanyika kabisa katika jamii iliyostaarabika. Naomba seneti kuchunguza kisa chenyewe kwa kina na wale watakaopatikana na hatia waadhibiwe. Haki za watoto sharti ziheshimiwe,” alisema Bi Kihika.
Baadhi ya mambo ambayo kamati ya seneti inalenga kuchunguza ni mahali walikoenda watoto watano ambao hawakupatikana baada ya wenzao kurejeshwa mjini Nakuru.
Watoto hao walidai kuwa askari wa serikali ya Kaunti ya Nakuru mnamo Februari 6 waliwavamia, wakawafunga pingu na kuwasafirisha kwa gari hadi eneo la Torongo, karibu na msitu wa Chemasusu ambapo waliachwa.
Walisema maafisa hao wa kaunti waliwakashifu kuwa walikuwa wakichafua mji na kuwahangaisha wakazi.