DAP-K yatangaza kujiondoa Azimio: ‘Hatuwezi kushirikiana na wasaliti’
MUUNGANO wa Azimio la Umoja-One Kenya unaendelea kupoteza nguvu baada ya chama cha Democratic Action Party of Kenya (DAP-K) kuwa chama cha hivi punde kutangaza nia ya kujiondoa.
Akiongea mwishoni mwa wiki, kiongozi wa chama hicho Eugene Wamalwa alisema chama hicho kimefikia uamuzi huo kutokana na kile alichokitaja kama usaliti kutoka kwa uongozi wa muungano huo.
“Kama DAP- K hatuwezi kuendelea kushirikiana na watu ambao wameamua kuwa watetezi wa serikali ya Kenya Kwanza inayowanyanyasa na kuwakandamiza raia. Hatuwezi kuendelea kushirikiana na watu ambao hatulandani kifikra na kisera,” Bw Wamalwa akawaambia wanahabari mjini Webuye, Kaunti ya Bungoma.
Waziri huyo wa zamani wa Ulinzi alidai kuwa baadhi ya vyama tanzu katika Azimio vinatumiwa na serikali kurejesha aina mbalimbali za ushuru za kuwaumiza Wakenya.
“Tumekubaliana na wenyeviti wa DAP-K kutoka kaunti zote 47 kwamba chama chetu kitaanza mchakato wa kujiondoa kutoka Azimio. Aidha, wataanzisha mchakato wa kuandikisha wanachama wapya kuandaa chama chetu kwa uchaguzi mkuu ujao. Hatuwezi kushirikina na watu wanapanga tena kuwaongezea Wakenya mzigo wa ushuru,” Bw Wamalwa akaeleza baada ya kuongoza mkutano wa Kamati ya Kuu ya Kitaifa (NEC) ya DAP-K.
Mnamo Julai 15, mwaka huu chama cha Narc-Kenya kitangaza nia ya kujiondoa Azimio baada ya kukerwa na ukuruba kati ya ODM na muungano wa Kenya Kwanza.
Siku chache baadaye, mnamo Julai 29, chama cha Party of National Unity (PNU) nacho kilisema kitajiundoa Azimio.