Dawa ya kupanga uzazi iliyopigwa marufuku yarejea sokoni
Na BERNARDINE MUTANU
Dawa ya kupanga uzazi kutoka China iliyopigwa marufuku miaka 10 iliyopita baada ya kugundulika kudhuru wanawake na watoto imerejea nchini.
Dawa hiyo inauzwa kisiri katika kliniki za kuuza dawa za kienyeji, bila bodi ya dawa na sumu (PPB) kujua.
Dawa hiyo inafahamika kama Sofia na inauzwa katika maeneo kadhaa nchini, na pia kupitia kwa mitandao ya kijamii.
Ni rahisi dawa hizo kupatikana kwani wauzaji wanaziwasilisha kwa wateja. Pia, bei yake ni ya chini sana kwani tembe moja ni Sh200.
Watumiaji wanahitaji tembe moja kwa mwezi ikilinganishwa na tembe za kupanga uzazi za kila siku, na ndio maana ni kivutio kikubwa kwa wanawake kwa upangaji wa uzazi.
Wafanyibiashara huuza dawa hizo haramu kwa kudai kuwa ni dawa za kienyeji. Hata hivyo zimeripotiwa kuwa na madhara mabaya kwa wanawake na watoto wanaonyonya.
Kulingana na utafiti uliofanywa, watumiaji huhisi kizunguzungu, kuathirika kwa matiti kuwa laini sana, kupigwa na moyo, miguu mizito, uchovu na hisia ya kuwa mjamzito.
Utaifiti uliofanywa na maabara ya kitaifa ya kudhibiti ubora (NQCL) ulibainisha kuwa dawa hizo zilikuwa na kiwango kikubwa cha homoni.
Kiwango kikubwa cha homoni ya uzazi ya ‘oestrogen’ husababisha damu kuganda na ugonjwa wa moyo kulingana na Dkt Jill Mutua, mfamasia wa hadhi ya juu.