Deacons East Africa kuwekwa katika usimamizi
Na BERNARDINE MUTANU
Duka la manguo la Deacons East Africa huenda likatolewa kwa usimamizi mpya kutokana changamoto za kifedha linalopitia.
Notisi kutoka kwa wasimamizi wa bodi ilisema kuwa hatua hiyo iliafikiwa Ijumaa wiki jana.
Bodi hiyo zaidi inatathmini ikiwa itamteua Peter Kahi na Atul Shah wa PKF Consulting kusimamia kampuni hiyo.
“Lengo kuu kutoa Deacons kwa usimamizi mpya ni kuhakikisha kuwa inafanya vyema kuwafaa wamiliki ikilinganishwa na ikiwa itatangazwa iliyofilisika,” alisema Mkurugenzi Mkuu wa Deacons Muchiri Wahome katika taarifa.
Deacons imeorodheshwa katika soko la hisa humu nchini (NSE) na imeendelea kukadiria hasara.
Katika muda wa miezi sita kufikia Juni 2018, ilikadiria hasara ya Sh229.5 milioni ikilinganishwa na Sh180.4 milioni katika muda huo 2017.
Hasara hiyo ilitokana na kufungwa kwa operesheni za Mr Price, hatua iliyoshukisha mapato kwa asilimia 20.7.
Mwaka huu, kampuni hiyo ilikuwa na mpango wa kuuza matawi manne, yote yaliyo Jijini Nairobi.
Deacons inauhusiano na familia ya Kibaki, ambapo bintiye, Judy Kibaki ni mmoja wa wakurugenzi wakuu wa bodi ya wasimamizi.