Habari Mseto

Diwani ailaani serikali ya kaunti kuwanyima walemavu ajira

April 30th, 2019 1 min read

Na GEORGE MUNENE

UONGOZI wa serikali ya Kaunti ya Embu Jumanne ulikashifiwa kwa kutowapa walemavu ajira huku ikibainika hakuna hata mlemavu mmoja aliyeajiriwa na kaunti hiyo kutoka mwaka wa 2017.

Kulingana na wawakilishi wa Wadi, walemavu wanahisi walibaguliwa kwa sababu nafasi zote 355 za ajira ziliwaendea watu wasio na ulemavu.

Diwani mteule Bernard Kandia alisikitikia hilo na kusema ni kinyume cha katiba inayohitaji asilimia tano ya wafanyakazi wote kwenye kaunti wawe walemavu.

Bw Kandia akitoa maoni yake kuhusu ripoti ya kamati ya bunge la kaunti kuhusu Uongozi na Utumishi wa Umma, alisema wakati umewadia kwa kaunti kuwathamini walemavu na kuwapa kazi kama binadamu wengine.

Mwenyekiti wa kamati hiyo Duncan Mbui ambaye ni diwani wa Evurore, alithibitisha kwamba hakuna mlemavu aliyeajiriwa mwaka 2017 lakini akawa na wakati mgumu kueleza sababu zilizosabibisha walemavu kunyimwa ajira.

Kati ya 355 walioajiriwa, kauntindogo za Manyatta, Runyenjes, Mbeere Kaskazini na Mbeere Kusini ni 149, 67, 61, 46 na 32 mtawalia huku 32 waliosalia wakitoka nje ya kaunti ya Embu.