• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 8:55 PM
Dkt Silverstein asema Moi alipenda divai kutoka Israel

Dkt Silverstein asema Moi alipenda divai kutoka Israel

Na SAMMY WAWERU

SAFARI ya urafiki wangu na Mzee Daniel Toroitich Arap Moi ilianza miaka 42 iliyopita, wakati akiwa Makamu wa Rais chini ya utawala wa Rais mwanzilishi wa taifa hili Hayati Mzee Jomo Kenyatta, alitoa ushuhuda Dkt David Silverstein.

Huyu alikuwa daktari wa karibu wa Rais huyo wa pili wa Kenya ambaye alizikwa Jumatano nyumbani kwake Kabarak, Kaunti ya Nakuru.

Silverstein alisema alikutana na Mzee Moi mnamo 1977.

“Wakati huo nilikuwa na umri wa miaka 33, na tukaanza urafiki wetu wa karibu uliodumu miaka 42,” Dkt Silverstein Jumatano aliambia waombolezaji.

Akitoa salamu zake za pole kwa familia, jamaa, marafiki na taifa kwa jumla, Dkt Silverstein alisema alisafiri na Mzee Moi katika kila kona ya dunia aliyozuru.

Daktari huyo alifichua kwamba Mzee Moi alipenda divai kutoka nchini Israel.

“Alifurahia divai kutoka Israel. Tukiwa watatu; Mzee Moi, Charles Njonjo nami, alitueleza hiyo ni dawa ya wazee,” akasimulia.

Kando na kumhudumia kimatibabu, Dkt Silverstein aliendelea kueleza “katika safari ya Mzee mataifa mbalimbali duniani alisisitiza nihakikishe tusile nyama zisizofaa kama vile za paka, nyoka na mbwa”.

Mnamo Jumanne katika ibada ya kumuenzi Moi, kitinda mimba wa Mzee Moi, Gideon Moi na ambaye pia ni Seneta wa Baringo, alifichua kwamba babake alipenda nyama choma hasa ile ya mbavu.

“Ningemweleza daktari amemkataza asili nyama, aliniuliza ‘unaona daktari hapa’,” Gideon alisimulia.

Mzee Moi alitawala Kenya kuanzia mwaka 1978 hadi 2002 na anakumbukwa kwa mengi hasa maendeleo, sekta ya elimu ikitajwa kama aliyotilia maanani zaidi.

Aliaga dunia wiki iliyopita, Februari 4, 2020, Nairobi Hospital.

Kwa kuwa amewahi kuhudumu kama Amiri Jeshi Mkuu, mazishi yake yalikuwa ya kitaifa na ya hadhi ya juu zaidi ambapo maafisa wa kijeshi walifyatua mizinga 19 kuonyesha heshima za mwisho kwa Rais huyo mstaafu.

Kiongozi wa nchi Uhuru Kenyatta aliongoza taifa katika kumpungia mkono wa buriani Mzee Moi.

You can share this post!

Joka lawasilishwa kama ushahidi

BBI: NCIC yataka nguvu za kuwashtaki na kuwaadhibu...

adminleo