Habari Mseto

DPP apewa mwezi mmoja kuamua ikiwa atamshtaki upya Wambua

December 23rd, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na Lillian Mutavi

Mahakama ya Kithimani, Kaunti ya Machakos imempatia Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) siku 30 kuamua iwapo atamshtaki upya James Wambua aliyeachiliwa huru baada ya kufungwa jela miaka 10 kwa kusingiziwa kunajisi binti yake.

Hakimu Eva Wambugu alitoa agizo hilo baada ya upande wa mashtaka kueleza kwamba haujaamua iwapo utapinga kuachiliwa kwa Bw Wambua.

Kesi hiyo ilitajwa mbele ya Bi Wambugu Jumatatu baada ya Jaji George Odunga aliyemwachilia Bw Wambua wiki jana kuagiza ianze upya.

“Nimechunguza ombi lao na hawako tayari kuwasilisha mashtaka au kukata rufaa kupinga uamuzi wa mahakama kuu na wanahitaji muda wa kuchunguza uamuzi huo kabla ya kufanya uamuzi,” alisema Bi Wambugu.

Alipatia DPP mwezi mmoja kufanya uamuzi. Bw Wambua yuko nje kwa dhamana ya Sh30,000 aliyopatiwa na Jaji Odunga wa mahakama kuu ya Machakos.Hakimu alisema kwamba kwa sababu kesi hiyo ni ya zamani inafaa kuchukua muda mfupi iwezekanavyo.

Wakili Cyrus Maweu anayemwakilisha Wambua alisema ni sawa kwa DPP kuomba muda wa kuchunguza uamuzi wa DPP. Kesi hiyo itatajwa Januari 25 2021.

Bw Wambua ameendelea kupata misaada kutoka kwa wahisani kumsaidia kuanza upya maisha yake baada ya kuachiliwa huru.Amepatiwa ardhi, pikipiki na simu ya kisasa.

Alikuwa amefungwa jela maisha kwa kumdhulumu kimapenzi binti yake mashtaka ambayo yalipangwa na mkewe.Binti huyo Dorcas Wambua alisema alilazimishwa na mama yake kumsingizia mashtaka na akamfunza ushahidi aliotoa kortini.