Duale atetewa dhidi ya lawama za kuchangia kushikwa kwa gavana wa Garissa
NA KNA
WAZEE kutoka ukoo wa Abduwak wamemtetea vikali kiongozi wa wengi bungeni Aden Duale dhidi ya madai kwamba yeye ndiye alichochea kukamatwa kwa Gavana wa Garissa Ali Korane.
Wazee hao waliwakaripia wale ambao wanajaribu kuchafua jina la Duale kwa kumhusisha na masaibu ya Korane wakidai watu hao wameshawishiwa kisiasa kufanya hivyo.
Wakiongozwa na Sultan Dekow Sambul wazee hao jana walipuuzilia mbali madai ya Bw Aden Gamadid kwamba Duale ndiye alichangia “kukamatwa na kuhojiwa” kwa Gavana Korane kuhusu kupigwa risasi kwa Waziri wa Fedha wa Kaunti ya Garissa Idriss Mukhtar.
Jana, Gamadid, ambaye alikuwa ameandamana na baadhi ya wazee, walitoa taarifa wakidai Duale ndiye alipanga kukamatwa kwa Korane.
Bw Idriss amelazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi katika Nairobi Hospital baada ya kupigwa risasi na mtu asiyejulikana alipokuwa akitoka msikiti mmoja jijini Nairobi.
“Ninataka kusema bila woga au kujikanganya kwamba Duale ndiye amesababisha haya yote. Amekuwa akimsumbua gavana na kumzuia kuendelea na majukumu yake. Ni kinaya kwamba Duale anampinga Gavana Korane ilhali ni yeye (Duale) alimpigia debe wakati wa uchaguzi mkuu uliopita,” Gamadid akasema.
Idriss alipigwa risasi mwezi jana katika mtaa wa Kileleshwa.
Gavana Korane alijitenga na jaribio hilo la kumuua Waziri Idriss huku akidai kuwa mahasidi wake wa kisiasa ndio walichochea kukamatwa kwake.