Dume lachoma mkewe kwa kukosa kumpikia githeri
Na GEORGE MUNENE
MWANAMKE amelazwa katika Hospitali ya Kirinyaga akiwa kwa hali mahututi baada ya kushambuliwa na mume wake katika mtaa wa mabanda wa Riverside, eneo la Ngurubani kwa kukosa kumpikia mlo anaopenda sana wa Githeri.
Bi Catherine Waithera, 27, alichomwa sana usoni na kifuani aliporushiwa stovu iliyomlipukia.
Baada ya shambulio hilo, mshukiwa Peter Ngugi, 32, alitoroka na polisi wanamtafuta.
Mwanamume huyo ambaye ni dalali wa tomato aliwasili nyumbani Jumamosi usiku akapakuliwa wali lakini akasisitiza apewe githeri.
Hata hivyo, Bi Waithera alimwambia mume wake hapakuwa na githeri na ilifaa ale chakula alichopikia kila mtu kwa familia.
Walianza kubishana lakini Bi Waithera akasema haingewezekana kupika githeri wakati huo wa usiku.
Hapo ndipo mwanamume huyo alichukua stovu iliyokuwa ikiwaka moto na kumrushia mke wake akaanguka.
Baada ya kutenda uovu huo, alitorokea mashamba ya mpunga yaliyo karibu na kumwacha mwathiriwa akigaagaa kwa uchungu na kuitisha usaidizi.
Wakazi waliomsikia walifika kwa haraka na kumpata mama huyo wa watoto wawili akiwa amechomeka sana wakampeleka katika Hospitali ya Comrade ambako alilazwa akiwa katika hali mahututi.
Bi Tabitha Wairimu ambaye ni jirani yao alisikia kilio na alipokimbilia nyumba hiyo alimkuta mwathiriwa akiwa amezimia sakafuni.
“Nusura nianguke kwa mshtuko nilipoona hali ya mwathiriwa,” akaongeza Bi Wairimu.
Mzee wa mtaa huo, Bw Antonu Mwangi alisema mshukiwa hupenda vita sana na huwa anampiga mke wake mara kwa mara.
Dkt Hikokha Aoka wa Hospitali ya Comrade alisema mwathiriwa alichomeka asilimia 15 mwilini lakini yuko thabiti.
Kaimu Mkuu wa Polisi wa Mwea Mashariki, Bw Luka Chebet alisema alifahamishwa kuhusu kisa hicho na polisi wameanzisha msako kumtafuta mwanamume aliyetoroka baada ya kutenda kitendo hicho cha unyama.
“Tunamtafuta mshukiwa na akipatikana atashtakiwa kwa kosa la uvamiaji,” akasema Bw Chebet.