EABL yatangaza kuongeza bei ya pombe
Na BERNARDINE MUTANU
Kampuni ya pombe ya East African Breweries Limited (EABL) imetangaza azimio la kuongeza bei ya pombe ikiwa Hazina ya Fedha itatekeleza pendekezo la kupandisha ushuru wa mashirika kutoka asilimia 30 hadi asilimia 35.
Pendekezo hili ni kwa mashirika yaliyo na mapato ya zaidi ya Sh500 milioni.
Meneja Mkurugenzi wa Kenya Breweries Jane Karuku alisema ongezeko la ushuru litatiza biashara, kufuatia kuwa sekta hiyo ni kati ya sekta zinazotozwa ushuru mwingi zaidi nchini.
“Ushuru wa asilimia 35 utatushtua na utakuwa mbaya zaidi kwa biashra, sisi ni kati ya kampuni zinazotozwa ushuru zaidi Kenya na eneo hili,” alisema.
“Kuongeza ushuru ni kumaanisha kuwa lazima tutapitisha kiwango fulani kwa wateja. Hili litafanya bei ya pombe aina ya Tusker kuongezeka kutoka Sh160 hadi kufikia Sh180 kwa sababu,” alisema.
Alisema hayo Jumatano kabla ya kampuni hiyo kuwasilisha maoni yake kuhusiana na marekebisho ya ushuru kwa Hazina ya Fedha kwa mwaka wa fedha wa 2019/2020.
Kulingana Bi Karuku, Sh87 kati ya Sh160 zinazouzwa pombe ni ushuru na kwamba ongezeko lolote la ushuru litawafanya wateja wa pombe za kiwango cha chini kuanza kubugia pombe haramu.
Akihutubia wanahabaro, Bi Karuku alisema ongezeko la ushuru likichanganywa na ongezeko la mfumko wa bei ya bidhaa litafanya aina tofauti za pombe kuwa ghali zaidi.