Habari Mseto

EACC yanyaka wakili, karani wa korti kwa kula rushwa

June 17th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

Na VICTOR RABALLA

MAKACHERO wa Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi Nchini (EACC) mnamo Ijumaa walinyaka wakili na karani wa mahakama kuhusiana na sakata ya hongo ambayo ililalamikiwa na Jaji wa Mahakama ya Kisumu, Roseline Aburili.

Wakili Clifford Odhiambo Gwada na karani huyo Zakayo Otieno Wambogo walikamatwa na kuendelea kuzuiliwa katika Kituo cha Polisi cha Railways.

Msemaji wa EACC, Eric Ngumbi, alisema walifahamishwa kuhusiana na suala hilo baada ya malalamishi ya Jaji Aburuli.

Jaji huyo alidai kuwa wawili hao walikuwa wamepokea Sh500,000 kutoka kwa raia wakimhadaa kuwa walikuwa wakimwakilisha kwenye kesi mahakamani.

“Kwa kuendea hongo, washukiwa hao walisema kuwa Jaji alikuwa amewatuma ili kutoa uamuzi wa mapendeleo katika kesi itakayoamuliwa Mei 17,2024,” EACC ikasema kupitia taarifa.

Jaji huyo aliandikisha taarifa na EACC akisema alipata habari kuwa Bw Gwada alikuwa amempa karani wa korti Sh500,000 ili aletewe bila ufahamu wake.

“Aliwahoji wawili hao mahakamani ambapo walikiri kupokea pesa hizo na kuzigawa wenyewe,” akasema Bw Ngumbi.

Uchunguzi wa awali ulibaini kuwa Bw Gwada alipewa pesa hizo na Kampuni ya wakili wa Peter Warindu ambaye walikuwa wamemteua kwa muda kuwa wakili wao katika kesi hiyo.