Habari Mseto

Eastleigh sasa yageuka kitovu cha mauaji, utekaji nyara wakazi wakijaa hofu

Na NYABOGA KIAGE, STEVE OTIENO November 19th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

MTAA wa Eastleigh unaovuma kibiashara jijini Nairobi umekumbwa na visa vya mauaji na utekaji nyara siku za hivi karibuni.

Hali hii imesukuma idara ya usalama kutuma maafisa wa polisi kushika doria katika maeneo ya makazi na maeneo ya kibiashara.

Hali ya wasiwasi imetanda miongoni mwa wakazi na wanabiashara kutokana na mauaji haya ya kikatili.

Juma lililopita, msemaji wa Huduma ya Kitaifa ya Polisi (NPS) Resila Onyango aliambia Taifa Leo kuwa idadi ya maafisa wa polisi imeongezwa kukabili hali hii.

“Tunashirikiana zaidi na wakazi lengo kuu likiwa kuhakikisha wanatoa maelezo kwa mamlaka ili kuongeza usalama katika eneo hilo,” Dkt Onyango alisema.

Mauaji ya mwanabiashara yaliyotekelezwa kwa bunduki na mtu aliyekuwa akiendesha pikipiki, kuuliwa kwa mwanaume mchanga ambaye alikamilisha shule ya sekondari miaka miwili iliyopita na mauaji ya watu watatu wa familia moja, ni visa vya hivi punde zaidi ambavyo vinachunguzwa.

Wiki iliyopita, Abdirahim Abdullahi Ibrahim, 25, alipigwa risasi nje ya jumba la DD Plaza na muuaji aliyenaswa na kamera ya CCTV kisha kukimbilia mafichoni.

Maafisa wa polisi wanamzuia mwanamke kwa jina Bi Amina Abdullah na wanaendelea kuwasaka washukiwa watatu zaidi kuhusiana na mauaji hayo.

Makachero wanamtafuta mwanamke anayeaminiwa kuwa mchumba wa mwanaume aliyeuliwa. Mwanamke huyo ametokomea tangu Ibrahim alipopigwa risasi.

Kulingana na familia na marafiki, Abdullahi na mwanamke huyo anayemiliki saluni, walikuwa katika uhusiano wa kimapenzi wa miezi minane.

Bw Abdirahman Mursal, kaka wa marehemu, ameshindwa kuelewa sababu ya kuuawa kwa kaka yake ambaye alimaliza kidato cha nne mnamo Machi 2022 katika shule ya upili ya Lami huko Moyale.

“Kaka yangu alimaliza kisomo cha sekondari hivi maajuzi na hakuwa amejiunga na chuo. Kwa nini mtu amuue kwa njia ya kikatili namna hii? Bw Mursal alishangaa.

Mnamo Oktoba 21, Bi Waris Daud, 38, binti yake wa umri wa miaka 12 Nuseiba Dahir na mpwa wake Bi Amina Abdirashad, 23, waliuawa na miili yao kutupwa sehemu tofauti.

Mwanaume raia wa Ethiopia Hashim Dagane Muhumed yuko kizuizini baada ya kukamatwa. Bw Muhumed ndiye mshukiwa mkuu.

Washukiwa wa mauaji waliokuwa na pikipiki walimpiga risasi mwanabiashara wa Eastleigh Bw Adan Ali Mohamed na kuiba Sh3.9 milioni mnamo Machi 26.

Siku chache baadaye, miili ya washukiwa hawa – Fredrick Kopo (Frik) na Jaylan Kibe – walionaswa na kamera za CCTV ilipatikana katika Mochari ya City pamoja na mwili wa mwanamke aliyesemekana kuwa rafiki wa karibu wa Kibe.

Zaidi ya hayo, Taifa leo imebaini kuwepo kwa makumi ya visa vilivyoripotiwa kuhusiana na ujenzi wa majumba eneo la Eastleigh.

“Tunapokea ripoti kila wiki za wajenzi kuanguka kutoka majengo marefu Eastleigh. Pia vifaa vya ujenzi vinaangukia wapitanjia,” Kamanda wa Polisi wa Kaunti Ndogo ya Starehe Fred Abuga alisema mnamo Mei 2024.