Elimu ya juu yafaa kuwa na ubora wa kimataifa – Prof Waudo
Na LAWRENCE ONGARO
MASOMO ya chuo kikuu yanastahili kufuata maagizo yaliyotengwa katika mtaala wake ili kuafikia kiwango cha kimataifa, ndiyo kaulimbiu ya Naibu wa Chansela wa Chuo cha Mount Kenya Profesa Stanely Waudo.
Alisema chuo hicho kimekuwa kikifuata utaratibu huo ili kufuatilia kikamilifu mpangilio uliowekwa masomoni.
Alitaja kukabidhiwa kwa cheti maalum cha ubora wa huduma cha ISO (Certified quality Management System), kama ithibati ya kutimiza ubora wa kimataifa.
Prof Waudo alisema kuwa mara ya kwanza chuo cha Mount Kenya kutambulika kutokana na cheti hicho cha ISO :9001 ilikuwa mwaka wa Desemba 19, 2012.
Ilipofika mwaka wa 2015 chuo hicho kwa mara nyingine kilitambulika kwa cheti cha ISO ,9001: 2015.
Alisema kufika katika kiwango hicho halikuwa jambo rahisi, kwa vile walilazimika kuleta pamoja washika dau na wasomi ili kupata mbinu mwafaka ya kupiga hatua zaidi za ubora.
“Chuo hiki kimepiga hatu kubwa kutokana na mikakati maalum iliyowekwa kwa mashauriano na wataalamu walio na ujuzi wa hali ya juu,” alisema Prof Waudo.
Chuo hicho kina mabewa zaidi ya manane hapa nchini na nchi jirani za Uganda na Rwanda.
Mwaka 2018, Baraza la Kitaifa la Uuguzi (NCK) lilitoa idhini kwa chuo hicho kuendesha somo la Afya huku likiwapa wauguzi mafunzo maalum.
Wengi wa wanafunzi hao huendesha mafunzo yao katika hospitali kuu ya Thika Level 5 kufuatia maelewano ya pamoja.
Wakati huo pia, idara ya sheria ilitoa idhini kwa chuo hicho kufunza stashahada ya uanasheria ambapo mafunzo hayo yanaendeshwa jijini Nairobi, eneo la Parklands.
Alieleza kuwa chuo hicho kinafuata maagizo yote yaliyowekwa ya kuona ya kwamba masomo yanayofunzwa huko yanaendeleza mataala na sheria zilizowekwa za masomo.
“Sisi tunafanya mikakati kuona ya kwamba kila mwanafunzi anayefuzu amechujwa vyema na wahadhiri wetu kuona ya kwamba kile walichofunzwa ni kamili na kinafikia kiwango cha kimataifa,” alisema Prof Waudo.