Habari Mseto

Familia 10,000 kunufaika na msaada Kiambu

June 3rd, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na LAWRENCE ONGARO

MADIWANI watakuwa miongoni mwa viongozi watakaosambaza chakula katika kaunti ya Kiambu.

Gavana wa Kiambu Dkt James Nyoro alisema ni vyema viongozi hao kupewa nafasi ya kusambaza chakula hicho kwa sababu wako mashinani.

Alisema kwa wakati huu chakula kipo kingi katika bohari la Ruiru, ambapo wanatarajia kushibisha zaidi ya familia 10,000 na chakula.

Dkt Nyoro aliyasema hayo mnamo Jumatano mjini Ruiru, alipotoa mgao wa chakula kwa madiwani wa maeneo tofauti ili wasambazie wakazi wa mashinani.

“Mpango huo tuliyozindua ni muhimu kwa sababu wananchi watapata chakula kwa njia ya uwazi bila ubaguzi,” alisema Dkt Nyoro.

Chakula kilichosambazwa ni unga wa ugali na chapati, vieuzi, Mchele na jezi za ( reflector).

Alisema homa ya covid-19, haijaangamizwa bado, na kwa hivyo ni lazima kila mmoja afuate sheria zilizowekwa na serikali ili kuikabili.

“Hivi karibuni tutazingatia upimaji wa covid-19 kwa kila mwananchi. Hiyo ni njia moja ya kukabiliana nayo,” alisema Dkt Nyoro.

Alisema mpango wa kaunti ya Kiambu ni kujiandaa vilivyo katika hospitali zote, huku wakilenga kuweka zaidi ya vitanda 1,000 katika wadi hizo.

Alieleza kuwa tayari wamefunga soko la Ngewa iliyoko Limuru, na ile ya Soko mjinga ili zipulizwe dawa ya kuangamiza viini vya covid-19.

Aliwasuta watu wanaochapa siasa wakati huu wa kusambaza chakula cha msaada.

“Mimi kama gavana wa Kiambu sitatishwa na maongezi ya watu kuhusu chakula cha msaada, bali nitaendelea na majukumu yangu muhimu ya kutumikia wananchi,” alisema Dkt Nyoro.

Alieleza kuwa huu ni wakati wa kutafakari kwa kina na kujiandaa kuendelea na maisha hata mambo yakirejea sawa baada ya covid-19.

Alisema Sh185 milioni zimetengwa za kufufua uchumi wa kaunti ya Kiambu kwa maendeleo.

Alieleza ya kwamba kwa muda wa mwezi moja lijayo barabara zote mbovu katika mashinani zitapata sura mpya ili kuboresha hali ya uchumi katika kaunti yote.

Alisema kila wadi katika kaunti itapokea zaidi ya Sh 1 milioni ili kutekeleza mabadiliko hayo.