Familia yalilia haki mwanaume akiuawa kikatili na watu wanaodaiwa kuwa polisi
MASWALI yamezuka baada ya mwanamme mmoja kuuawa na watu wanaoshukiwa kuwa maafisa wa polisi katika Kaunti ya Nakuru huku familia yake ikidai haki.
Bw Mathew Letyo, 35, aliaga dunia baada ya kupigwa risasi tumboni na watu wanne waliovamia makazi yake katika kijiji cha Bararket, Kuresoi, Nakuru.
Akizungumza Jumatatu na Taifa Leo, mkewe marehemu Cynthia Chepkemoi, alisimulia jinsi washambulizi hao walivyovamia makazi yao wakiwa wamelala usiku saa nne, wakavunja lango na kuwashurutisha kufungua.
Katika tukio hilo Oktoba 8, Bi Chepkemoi anasema wavamizi hao aliogundua baadaye ni maafisa wa polisi, waliitisha kuzungumza mumewe bila kusema walichohitaji.
Wote wanne walianza kumzomea Letyo mbele ya mkewe lakini akafanikiwa kuchomoka kabla ya watatu kumfuata mbio na kumkamata.
Chepkemoi alisema alisikia milio ya risasi dakika chache tu baada ya mumewe kuwasihi maafisa hao kuokoa maisha yake.
Inadaiwa marehemu alipigwa risasi tumboni kabla ya washambulizi kumburura chini kwa umbali wa mita 50 hadi langoni ambapo mwendeshaji bodaboda alikuwa anasubiri.
“Baada ya milio ya risasi nilijua hayupo tena. Tulikuwa tumekaa siku nzima pamoja. Alikuwa na mipango mingi kuhusu familia yetu. Mipango ya kupanua chumba ndani ya nyumba yetu ili iwe na nafasi ya mgeni. Inahuzunisha kuwa walikatiza maisha yake,” alisema mama huyo akibubujikwa na machozi.
Maafisa hao kisha walirejea na kusaka nyumba hiyo kabla ya kuondoka na Sh10,000, panga, uta na mshale wakidai Letyo alitaka kuwashambulia.
Bi Paulina Kipsimian, mamake marehemu anasema alipigiwa simu na mkaza mwanawe saa tano usiku akimfahamisha kilichotokea.
Kipsimian, ambaye ni mkazi wa Kongasis, Gilgil anasema Chepkemoi alimweleza maafisa hao walimfunga pingu Letyo kabla ya kumpigia risasi na kumburura.
“Nataka mwanangu afanyiwe haki, walimuua ilhali hakuwa na hatia. Baadaye nilifahamishwa alikuwa ameripitiwa na jirani aliyedai Letyo aliachilia ng’ombe wake kula nyasi yake. Aliripoti suala hilo kwa polisi. Sijui kama aliuawa sababu hiyo,” alisema.
Kaka yake Letyo, Noah Chesire, alisema marehemu alizozana na jirani yake mwezi mmoja uliopita baada ya ng’ombe wake kuingia shamba lake.
Ingawa polisi hawakuzungumzia suala hilo walipomshambulia, familia yake inauliza ikiwa hiyo ndiyo ilikuwa sababu.
“Hatujui ikiwa aliuawa kwa sababu ya mtafaruku huo au nini alichofanya kustahili kifo cha uchungu hivyo. Tunachotaka ni majibu na yeyote aliyefanya hivyo achukuliwe hatua,” anasema.
Jumapili, familia na marafiki walikusanyika nyumbani kwake Chepkemoi kushiriki maombi na kupanga mazishi huku wakiitisha haki.
Kamanda wa Polisi Kuresoi Kusini Jeremiah Leariwala alisema uchunguzi umeanzishwa kuhusu tukio hilo.
Makachero kutoka Idara ya Uchunguzi kuhusu Uhalifu, DCI, wamechukua suala hilo na kufikia sasa mashahidi wameandikisha taarifa.