• Nairobi
  • Last Updated April 30th, 2024 3:55 PM
Familia yamlilia Boinnet kuokoa jamaa yao aliyetekwa nyara

Familia yamlilia Boinnet kuokoa jamaa yao aliyetekwa nyara

NA PETER MBURU

FAMILIA moja kutoka kaunti ya Nakuru inamtaka Mkuu wa Polisi Joseph Boinett kuwasaidia kumpata mmoja wao ambaye anadaiwa kutekwa nyara na watu waliojidai kuwa maafisa wa polisi.

Bw Fredrick Kinanga, mfanyabiashara wa mbao alichukuliwa kutoka nyumbani kwake usiku wa Jumanne saa mbili, na wanaume wanne waliojitambulisha kuwa wa kutoka idara ya upelelezi.

Watu wa familia yake walieleza Taifa Leo kuwa wanne hao, ambao hawakuwa na sare ya kazi wakati wa tukio hilo lakini walikuwa na pingu walifika nyumbani kwa Bw Kinanga na kuamrisha kuondoka naye.

Mkewe mfanyabiashara huyo, Bi Lilian Chemutai alisema walimtafuta mumewe kuanzia usiku wa manane na hata walipofika kituo cha polisi cha Nakuru Central hawakumpata, japo walibaini kuwa alifikishwa humo na kuondolewa saa tisa alfajiri.

“Tulifika kituoni saa kumi na tukafahamishwa kuwa alipelekwa Kisii, ijapokuwa mitambo ya kufuatilia simu ilionyesha kuwa alikuwa eneo karibu na Nairobi,” Bi Chemutai akasema.

Familia hiyo sasa inahofia mpendwa wao kuuawa mikononi mwa polisi na hivyo kuwataka Bw Boinett na mkuu wa upelelezi kuwasaidia kumpata.

“Tunashindwa kuelewa suala hili kwani ni vibaya zaidi. Ni mume na baba ya watu. Tunatumai kuwa serikali itachukua hatua zifaazo,” akasema mjomba wake Bw Job Mochache.

“Tunahofia ikiwa hawa walikuwa polisi wa kweli, inawezekanaje kukaa na mtu kwenye gari kama mzigo kwa saa 24, kuna hatua za kufuata kisheria ikiwa amekosea kama kumfikisha kortini,” Bw Mochache akaongeza.

Familia hiyo haikuelewa sababu ya mfanyabiashara huyo kupelekwa Nairobi na maafisa waliodaiwa kutoka Kisii, na kukosa kutoa habari.

Wakili wa familia hiyo Bw Gordon Ogolla alishuku nia ya watu hao, na kutaka kufahamu kwanini polisi katika kituo cha central hawakutoa habari.

“Kwa kuzingatia mambo yalivyo nchini kwa sasa, kuwa katika mikono ya maafisa wasiofahamika na wasiotoa habari ni hatari, tunasubiri kuambiwa kuwa mwili wake umepatikana sehemu fulani sasa. Kabla ya hilo kutendeka, tunawaomba Bw Boinett na idara ya polisi kuhakikisha kuwa Bw Kinanga amepatikana,” akasema Bw Ogolla.

Hata hivyo, akijibu madai ya kuzuiliwa katika kituo cha polisi cha central saa 11 tangu jamaa huyo kuondolewa kituoni, mkuu wa polisi Nakuru mjini (OCPD) Bw Samuel Obara hakutoa habari zozote, akisema “Si kazi yangu kwenda kituoni kuitisha habari kuhusu kisa Fulani, nasubiri kuletewa ripoti ndipo nifahamu kuwa jambo limetendeka.”

You can share this post!

Wanne waitwa kuwasaidia Lionesses kutamba Botswana

KRA yazuilia watu 21 wa kigeni waliotwaa magari kutoka kwa...

adminleo