Habari Mseto

Familia yasisitiza kifo cha ‘Shirandula’ kingeepukika

July 20th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na SHABAN MAKOKHA

FAMILIA ya aliyekuwa muigizaji wa vipindi vya runinga, marehemu Charles Bukeko imelaumu Hospitali ya Karen, Nairobi kwa kifo chake.

Ikiongozwa na babake Cosmas Wafula na mkewe Beatrice Andega, familia hiyo inataka hospitali hiyo kutoa taarifa ya kina kuhusu chanzo cha kifo cha Bukeko, aliyefahamika kwa msimbo Papa Shirandula.

Mwigizaji huyo alizikwa Jumatatu asubuhi nyumbani kwake katika kijiji cha Namisi-Bukeko eneo la Funyula, Kaunti ya Busia katika mazishi yaliyochukua saa moja pekee. Bi Andega alilaumu madaktari wa hospital ya Karen kwa kumpuuza mumewe.

“Tulipoenda katika hospitali hiyo, aliomba afanyiwe uchunguzi wa magonjwa matatu ambayo ni Malaria, Niumonia na Covid-19 lakini hospitali hiyo ilipima corona pekee na kukataa vipimo vingine,” Bi Andega alisema.

Bw Wafula alikanusha kuwa, mwanawe aliuawa Covid-19 akafichua familia inapanga kuteua wakili kufuatilia suala hilo.

“Kwa sasa, siwezi kusema chochote kuhusu ugonjwa wake hadi tutakaposhauriana na hospitali hiyo,” Mzee Wafula alisema.Mwili wa Papa Shirandula ulizikwa saa mbili na dakika arobaini na tano, saa tano baada ya kuwasili nyumbani kwake kutoka Nairobi.

Hata hivyo, Afisa Mkuu Mtendaji wa Hospitali ya Karen, Bi Juliet Nyaga, jana aliyapuuzilia mbali madai ya familia hiyo akisema hospitali hiyo inasifika kwa utoaji huduma za hali ya juu kwa wagonjwa.

“Wahudumu katika Hospitali ya Karen wameendelea kutoa huduma za hali ya juu kwa Wakenya hata wakati wa janga la Covid-19 wakizingatia kanuni za Wizara ya Afya na Shirika la Afya Ulimwenguni,” akasema kwenye taarifa.

Mazishi yalitanguliwa na ibada fupi iliyofanyika chini ya usimamizi wa maafisa wa afya na usalama. Baada ya mwili kuzikwa, waombolezaji wote waliagizwa kuondoka bomani.

Wanakijiji waliorauka mapema wakitarajia kuhudhuria mazishi walizuiwa kuingia katika boma na maafisa wa usalama.

Waigizaji wenzake wakiongozwa na Jackline Nyamide, almaarufu kama Wilbroda aliyeigiza kama mke wa Bukeko katika kipindi cha Papa Shirandula, walisema marehemu alikuwa kama baba na mlezi wa vipawa katika tasnia ya uigizaji.

Wilbroda aliibua kicheko kwa waombolezaji aliposema hata mke wa Bukeko alikuwa anamfahamu kama mke wa pili katika boma hilo.