Faraja wakazi kupata haki baada ya miaka 50
Na LAWRENCE ONGARO
WAKAZI wanaoishi kwa ardhi ya Gachagi mjini Thika, walipata haki yao baada ya mahakama moja ya Thika kuwaruhusu waendelee kumiliki ardhi hiyo.
Mwenyekiti wao Bw Simon Kibe Mwangi, alisema hiyo ilikuwa ni afueni kwa sababu wamekuwa kama wakimbizi katika ardhi hiyo kwa zaidi ya miaka 50.
“Sisi kama wakazi wa eneo hilo la Gachagi tunaipongeza Mahakama ya Thika kwa kuonyesha haki kwetu. Hiyo ilikuwa ni sauti ya Mungu iliyoshuka kwetu na kwa hivyo tutaendelea kumtukuza,” alisema Bw Mwangi.
Alisema eneo wanakoishi kwenye ardhi hiyo ni ekari 40, lakini kipande chenyewe ilikuwa ekari 200.
Mkazi mwingine Bi Pauline Wangui aliyeishi eneo hilo kwa zaidi ya miaka 35 alisema utukufu wa Mungu ulionekana na kwa hivyo Mahakama ilifanya kweli kutoa uamuzi wa haki ulioridhisha kila mmoja wetu aliyehudhuria kesi hiyo.
“Tumekuwa tukizozania ardhi hiyo na mabwanyenye wenye pesa ndefu, lakini kwa sababu mnyonge pia ana haki yake, leo tumepokea kilicho chetu,” alisema Bi Wangui.
Kesi hiyo ambayo imejikokota kwa muda wa miaka 14 ilitamatishwa kirasmi na Jaji wa mahakama ya Thika, Bi Lucy Mbugua, ambaye kwa uamuzi wake alisema maskwota hao ambao wameishi kwenye eneo hilo kwa miaka 50 wana haki sasa kirasmi kulimiliki kama wenyeji.
Zaidi ya wakazi 100 walifurika katika Mahakama hiyo ili kupata haki yao ambayo imekuwa imebanwa kwa muda huo wote.
Alisema wale wanaodai kuwa shamba hilo ni lao kwa sasa hawana tena mamlaka kuumiliki
“Kwa hivyi nimetoa uamuzi ya kwamba maskwota walioishi katika shamba hilo kwa muda huo wote wana haki kamili ya kuumiliki kirasmi,” alifafanua wakati wa kukamilisha uamuzi wake.
Wakili wa kikundi hicho Bw Ishmael Nguring’a alisema kwa sababu sasa maskwota hao wanahaki kamili ya kuishi pale bila matata wana haki sasa ya kutafuta haki miliki kamili ili kila mmoja awe na pahali pake pa kuishi na kulima.