Habari Mseto

FASHENI: Amazon kuundia wateja apu ya kujipima mavazi

January 29th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

MASHIRIKA Na PETER MBURU

KAMPUNI ya mauzo ya mitandaoni Amazon inapanga kuunda programu ya simu ya fasheni ambayo itawezesha watu kujipima mavazi japo si moja kwa moja.

Apu hiyo itahitaji kuwa na ufahamu wa mambo ya kimsingi ya mtu na itakagua picha za mteja kupitia mitandao ya kijamii, kisha kupendekeza mavazi ambayo yanaweza kumfaa zaidi..

Baada ya ukaguzi huo, kampuni hiyo itapendekeza nguo ambazo mteja anaweza kufurahia. Apu hiyo aidha itapendekeza mavazi ya mtu kulingana na anga anamoishi na kazi anayofanya.

Baada ya kupendekezewa, wateja wa Amazon watakuwa na fursa ya aidha kuzikubali ama kuzikataa. Wateja aidha wataweza kutafuta nguo zaidi ambazo apu imewapendekezea.

Mkurugenzi wa ubunifu katika kampuni hiyo ya mauzo Mark Howell alieleza kuwa kiwango cha habari ambacho teknolojia hiyo itaunda ni kingi sana.

“Kwa kupitia picha za mteja, kampuni inaweza kuona wanachovaa, wanachoendesha n ahata ndani ya nyumba zao ili kubashiri kitu ambacho mteja anawezakupenda sana kukinunua,” Howell akasema.

“Itakagua picha ili kubaini sehemu za mwili ambazo zitaunda taswira nzuri,” akaongeza.

Apu hiyo sasa imeanza kuhofiwa kuwa huenda ikawa mwanzo wa mwisho wa biashara za ushonaji mitaani.

Mnamo Novemba 2018, utafiti ulionyesha kuwa biashara 2,692 za ushonaji zilifungwa kwa kipindi cha miezi sita.