Habari MsetoSiasa

Gavana ajitolea kushauri 'mbunge mlevi'

July 7th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na ERIC MATARA

GAVANA wa Nakuru Lee Kinyanjui amejitolea kumshauri Mbunge wa Molo Francis Kuria Kimani, ambaye aljitokeza akiwa mlevi chakari katika hafla iliyoandaliwa kutafuta suluhu ya ulevi eneobunge lake mwishoni mwa wiki iliyopita.

Gavana Kinyanjui alisema yuko tayari kumpa ushauri utakaomfaa mbunge huyo kutekeleza majukumu yake ipasavyo.

Bw Kimani, 30, Alhamisi alishangaza wakazi wakati alifika katika hafla hiyo eneo la Elburgon akiwa mlevi, licha ya kuwa ilinuiwa kutafuta suluhu ya unywaji pombe. Hata hivyo alijutia kitendo chake baadaye na kuomba wakazi msamaha.

Gavana huyo jana alisema tukio hilo lilikuwa la kusikitisha, lakini akawarai wakazi kutomchukia kwa msingi wa tukio moja tu.

“Haikufaa, lakini ni vizuri kufahamu kuwa viongozi pia ni binadamu. Kama kiongozi mkuu eneo hili, nitamshauri ili atekeleze majukumu yake ipasavyo. Uongozi ni safari, bora tu awe tayari kuelekezwa,” akasema Bw Kinyanjui.

Spika wa kaunti hiyo Joel Kairu pia Jumamosi aliwataka wakazi kumsamehe mbunge huyo, wamwombee na wampe fursa ya pili.

Mkutano wa umma ambao ulifaa kuongozwa na Naibu Kamushna wa Kaunti eneo la Molo David Wanyonyi uliisha kwa kusambaratika wakati mbunge huyo alijitokeza akiwa mlevi, akiwa na wasaidizi wake na kundi la wafuasi.

Wakazi walighadhabika kwani walitaka kupata suluhu baada ya unywaji pombe kudaiwa kusababisha vifo vya zaidi ya watu watano kwa miezi michache iliyopita.

Wakazi waliokuwapo walisema alipoalikwa katika jukwaa, mbunge huyo alianza kuyumba kutokana na ulevi.

Aliondolewa na polisi na maafisa wake wa usalama, wakati wakazi wenye ghadhabu walikuwa wakitishia kumuadhibu kwa tabia yake ya aibu.

Mbunge huyo wa mara ya kwanza alimbwaga Jacob Macharia aliyekuwa mbunge katika uchaguzi wa 2017, baada ya kuvutia maelfu ya wapiga kura.