Habari Mseto

Gavana aomba watahiniwa waliofurushwa Mau wasaidiwe

October 30th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na ANITA CHEPKOECH

Gavana wa Kericho Paul Chepkwony ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya elimu ya Baraza la Magavana, ameiomba serikali ya kitaifa kuwasaidia watahiniwa walioathiriwa maskwota walipofurushwa kutoka msitu wa Mau.

Bw Chepkwony alisema ghasia zilizotokea eneo hilo ziliathiri masomo ya watahiniwa wa mtihani wa darasa la nane (KCPE) na wa kidato cha nne (KCSE) ambao hawakupata muda wa kutosha kujiandaa kama wale wa maeneo mengine.

“Serikali inafaa kuwasaidia wanafunzi hawa kwa kuhakikisha watapata nafasi katika shule za kitaifa inavyotendeka kwa wanaotoka maeneo yaliyo nyuma kimaendeleo,” Gavana Chepkwony alisema kwenye taarifa.

Alisema wanafunzi wanafaa kujiandaa kwa mitihani katika mazingira tulivu kama wale wa maeneo mengine nchini. Kamishna wa Kaunti hiyo Muhktar Abdi alisema usalama umeimarishwa katika vituo vyote vya kufanyia mitihani ili kuzuia visa vya udanganyifu.