Habari Mseto

Gavana atishia kupiga marufuku tuktuk

May 14th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na WINNIE ATIENO

GAVANA wa Mombasa ametishia kupiga marufuku shughuli za usafiri kwa kutumia tuktuk na bodaboda kufuatia utovu wa usalama.

Aidha, alisema marufuku hayo yatalenga maeneo hatari ambapo wahalifu wanatumia tuktuk na bodaboda kuhangaisha wakazi wa Mombasa.

Akiongea kwenye hafla malaum ya kuhimiza wakazi kupanda miti siku ya Jumamosi, Bw Joho alisema changamoto za usalama zingalia tishio kubwa katika kaunti hiyo ya kitalii.

“Bombolulu, Mvita na Kisauni ni maeneo ambapo wahalifu wanaotumia tuktuk na bodaboda wanaendelea kuhangaisha wakazi. Wakazi wa maeneo hayo wanaishi wka hofu ya ushambulizi, lazima tukomeshe uhalifu hata kama ni kupiga marufuku basi tutafanya hivyo,” akasema.

Alisema watakaopinga hatua hiyo wataandamana lakini baadaye watazoea. Bw Joho alisema suluhu la utovu wa usalama ni sharti ipatikane.

“Ni majuzi tu ambapo jamaa mmoja hapo Tononoka alishambuliwa na mshukiwa akahepa kwa tuktuk. Nimepata habari kuwa visa vingi vya uhalifu vinatekelezwa na watu wanaohepa kwa kutumia tuktuk,” akaongeza.

Gavana huyo aliwalaumu baadhi ya madereva wa tuktuk na bodaboda kwa kuchangia katika utovu wa usalama akisisitiza kuwa wanashirikiana na wahalifu kuibia wakazi.

“Kwanini visa vya watu kushambuliwa na wakora wanaotoroka kwa tuktuk vinahushudiwa maeneo ya Mvita na Kisauni? Wakazi wamechoka na uhalifu na ni sharti usalama udumishwe. Hata mkiandamana mwishowe mtalala lakini lazima tupate suluhu,” akasema Bw Joho.

Bw Joho alitamka hayo siku kadhaa baada ya jamaa mmoja kushambuliwa na genge la majambazi waliohepa kwa kutumia tuktuk mnamo Ijumaa.

Aliwataka madereva wa tuktuk kuwataja wenzao ambao wanaendelea kushirikiana na wahalifu.

Viongozi wa dini wa baraza kuu la waislamu nchini (Supkem) walitoa wasiwasi wao kuhusiana na uhalifu huko Mombasa.

“Tuna wasiwasi sababu ya kuongezeka wk auhalifu Mombasa. Tunapoelekea Ramadhan tunataka vyombo vya usalama vikabiliane na utovu huo,” akasema mwenyekiti wa baraza hilo eneo la Pwani Sheikh Muhdhar Khitamy.