Habari Mseto

Gavana Kiraitu akana kuwashauri wakulima wasipande miraa

October 8th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na GITONGA MARETE

GAVANA wa Kaunti ya Meru, Bw Kiraitu Murungi, amepuuzilia mbali madai kwamba aliambia wakulima wa miraa waache kupanda mmea huo.

Akihutubia wakulima kutoka kaunti zote ndogo za eneo hilo mwishoni mwa wiki, Bw Murungi alisema hajawahi kuwaambia wakulima wang’oe mimea yao ya miraa, lakini yeye huhimiza wakulima kupanda pia mimea mingine mbali na kutegemea miraa pekee.

Alizungumza wakati aliposambaza miche 400,000 ya parachichi na makadamia, iliyogharimu Sh90 milioni.

Gavana huyo amekuwa akishinikiza upandaji wa aina tofauti za mimea ili kulinda wakulima kutokana na athari mbaya za kutegemea aina moja pekee ya mazao.

“Yeyote anayeeneza uvumi kwamba sitaki wakulima wapande miraa anawadanganya na hampaswi kufuata siasa hizo duni. Makadamia na parachichi zinaweza kupandwa vyema pamoja na miraa ili mpate mapato zaidi kwa sababu kile mnachohitaji ni pesa,” akasema.

Gavana huyo aliongeza, “Tunapeana miche bila malipo kwa wale wanaotaka na hatutalazimisha mtu yeyote. Wale ambao hawataki hela zaidi mifukoni wanaweza wakaachana na miche hii.”

Kwa upande wake, Naibu gavana, Bw Titus Ntuchiu alisema kilimo cha makadamia kimekuwa chenye faida kubwa kwani bei hufika hadi Sh200 kwa kilo moja ya zao hilo.

Naibu huyo aliwaeleza wakulima huku akiwashauri kukumbatia mmea huo.

“Katika msimu huu, wakulima walipata Sh53 milioni kutoka kwa makadamia na tunatarajia kuwa katika miaka mitano ijayo, mapato yatakuwa zaidi ya Sh600 milioni,” akasema Bw Nkuchiu, ambaye pia ni waziri wa fedha katika kaunti hiyo.