Habari MsetoSiasa

Gavana Mutua ataka kafyu ianze saa kumi na moja jioni

April 1st, 2020 Kusoma ni dakika: 1

NA SAMMY WAWERU

Rais Uhuru Kenyatta anafaa kubadilisha muda wa kafyu ili kusaidia kudhibiti kuenea kwa ugonjwa wa Covid – 19, amependekeza Gavana wa Machakos Dkt Alfred Mutua.

Kulingana na Dkt Mutua maambukizi ya ndani kwa ndani yaliyoripotiwa kuendelea miongoni mwa Wakenya, yatadhibitiwa ikiwa muda wa kutangamana utapunguzwa.

Hata ingawa gavana huyo ameungama kafyu si jambo rahisi kutekeleza, amemtaka Rais Kenyatta kupunguza muda wa kafyu kuanza na kuongeza saa za asubuhi.

Amri ya kutotoka nje kati ya saa moja jioni hadi saa kumi na moja asubuhi kila siku ilianza kutekelezwa Machi 27, Rais akisisitiza sharti kila mwananchi aitii.

“Ninamsihi Rais abadilishe muda wa kafyu, ianze saa kumi na moja za jioni hadi saa mbili asubuhi. Mambo yasipobadilika, atathmini muda huo na kuuongeza zaidi,” akasema Dkt Mutua mnamo Jumatano.

Kwenye mahojiano na kituo kimoja cha runinga, gavana Mutua hata hivyo amewataka Wakenya kuweka akiba na kwenye maghala vyakula, endapo muda wa kafyu utaongezwa hawatahangaika njaa.

Wakati huu taifa linapitia magumu katika oparesheni dhidi ya Covid – 19, uchumi ukidorora kwa kiwango kikuu, Dkt Mutua alihimiza wenye uwezo kimapato na kifedha kusaidia wasiojiweza kwa kuwapa vyakula.

“Si wote wanaopaswa kupata msaada, kuna matajiri ambao wanafaa kusaidiana na serikali kulisha wasiojiweza. Tuwe wazalendo,” akasema.

Rais wa Rwanda Paul Kagame ameonekana akisambaza vyakula kwa raia wa nchi hiyo wasiojiweza, kufuatia athari za Covid – 19.

Taifa jirani la Uganda linaendelea kutekeleza amri ya kutotoka nje siku nzima ili kudhibiti maenezi ya virusi hatari vya corona. Nchi nyingine Barani Afrika iliyotangulia na kuchukua mkondo huo ni Afrika Kusini.