Habari Mseto

Genge laibuka la wahudumu wa boda linalowinda wezi wa pikipiki hadi nchi jirani

Na DOMINIC OMONDI October 14th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

WAHUDUMU wa bodaboda wamekashifiwa kwa kuvunja sheria na kuvuka mpaka wa Kenya na Uganda kuwaua kinyama watu ambao wanashuku wameiba pikipiki zao.

Wizi wa pikipiki umekithiri sana kwenye mpaka wa Kenya na Uganda kwenye mji wa Busia. Vitengo vya kiusalama navyo vimedaiwa kuchangia hali hiyo kwa kujikokota kwenye uchunguzi ambao unastahili kuwahusisha polisi kutoka Kenya na wenzao kutoka Uganda.

Andre Lomilo Husim, raia wa Uganda ambaye anaishi mita 150 kutoka kwa mpaka wa Kenya na Uganda ni kati ya wale ambao waliuawa kinyama kwa tuhuma ya kuiba pikipiki.

Genge la wahudumu wa bodaboda walitumia njia zisizotambulika za kuingiza bidhaa za kimagendo (panya route) kama saruji na sigara kufika kwake upande wa Uganda.

Walipofika nyumbani kwake, walitumia jiwe kubwa kuvunja mlango na kumpata akiwa na mkewe. Kwa mujibu wa mkewe marehemu akiongea na Daily Monitor, genge hilo lilimtaka mumewe atoe pikipiki ambayo alikuwa ameiba na alipokosa kufanya hivyo, walimpiga.

Baadaye walimfunga kwa mkono kwenye pikipiki kisha wakamburura kwenye barabara hadi upande wa Kenya. Hapo walimuua na kuacha mwili wake ukiwa katika hali mbaya barabara ya Kiwanja-Ndege, mwili huo ukipelekwa kwenye chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Rufaa ya Busia-Kenya.

Siku ambayo Husim aliuawa, Mganda mwengine anayefahamika kama Wandera naye alikwepa kifo kupitia tundu la sindano.

Alitekwa na genge hilo kwa tuhuma ya kuiba pikipiki lakini akaokolewa na polisi kutoka Kenya.

Mwenyekiti wa wahudumu wa Bodaboda katika kituo cha Bubango Kevin Were ameshutumu polisi kwa uzembe kutokana na wizi wa pikipiki na akasema wezi hao hawafai kusamehewa.

Bw Were ambaye nyumbani kwake ni karibu sana na Uganda anasema watu wengi wameuza ngombe na mali yao kununua pikipiki hizo.

“Unauza ng’ombe kisha pikipiki uliyonunua inaibwa na mtoto wako anakosa karo ya kuenda shule. Ukikutana na aliyekuibia utamwacha? Wengine wanaiba kimabavu tu ndiposa wahudumu hukusanyika na kulipiza kisasi,” akasema Bw Were.

“Machifu na wazee wa vijiji maarufu kama Liguru hawatusaidii. Utawaona tu wakati serikali imeleta chakula cha msaada wakiwaita watu waende wachukue chakula,” akaongeza Bw Were.

Hata mpango wa Nyumba Kumi ambao ulianza kazi wakati wa utawala wa Rais mstaafu Uhuru Kenyatta ambapo angalau watu 10 wanaoishi karibu hufahamiana kwa lengo la kupunguza uhalifu, haujasaidia.

Pikipiki za Kenya ambazo zinaibwa na kupelekwa Uganda zina thamani kubwa sana huko ndiposa wizi huo umekithiri sana upande wa Kenya.

Si Busia pekee wizi wa bodaboda pia upo maeneo ya mipakani ya Isbania kwenye Kaunti ya Migori na Namanga katika gatuzi la Kajiado.

Polisi ambaye amehusika na visa vingi vya wizi wa pikipiki kule Isbania mpaka wa Kenya na Tanzania alisema tatizo ni kuwa wengi wana uraia wa mataifa hayo mawili.

“Wakishiriki uhalifu hapa wanakuwa raia wa Tanzania. Wote hapa wanatoka jamii ya Kuria ambayo inapatikana nchi hizo mbili, wanazungumza lugha na wana jamaa zao Tanzania na upande wa Kenya,” akasema polisi huyo ambaye hakutaka jina lake linukuliwe.

Afisa huyo anasema kuna genge ambalo limejipanga kiasi kuwa baadhi ya pikipiki zinaibwa hadi katika Kaunti ya Kisii.

Kufuatia kuongezeka kwa visa hivyo, wito umetolewa kwa vyombo vya usalama kutoka miji ya mipakani ya Tanzania, Kenya na Uganda, viwe ange na vishirikiane kumaliza tatizo hilo la wizi wa bodaboda.