Githu Muigai apewa miezi mitatu kujiandaa kwa kesi ya Anglo-Leasing
Na RICHARD MUNGUTI
HAKIMU mwandamizi Bi Martha Mutuku Jumatano alikashifu afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) kwa kutowapa nakala za mashahidi washtakiwa katika kesi ya kashfa ya Anglo-Leasing iliyopelekea serikali kupoteza zaidi ya Sh6.8 bilioni.
Bi Mutuku alisikitika sana kiongozi wa mashtaka Victor Mule akiungama kwamba aliwapa washtakiwa nakala za mashahidi Jumanne alasiri ilhali kesi ilikuwa imeorodheshwa kusikizwa Jumatano asubuhi.
“Nakubaliana na washtakiwa Deepak Kamani, Rashmi Kamani, waliokuwa makatibu Joseph Magari, Dave Mwangi kwamba hawakupewa muda wa kutosha kujiandaa kuwakabili mashahidi walioorodheshwa kutoa ushahidi Jumatano,” alisema Bi Mutuku.
Mwanasheria mkuu Prof Githu Muigai na wakili mkuu wa Serikali Muthoni Kimani aliye pia mkurugenzi wa Idara ya Usakaji Mali iliyonunuliwa na kodi ya wananchi walikuwa wameorodhesha kutoa ushahidi jinsi walipokea ushahidi dhidi ya washtakiwa kutoka nchini Uswizi 2009.
Prof Muigai alipokea ushahidi kutoka kwa Serikali ya Uswizi kuhusu kashfa hiyo. Alitarajiwa kueleza kilichojiri kuanzia wakati huo.
Kabla ya kesi hiyo kuanza mawakili Paul Nyamondi, Kioko Kilukumi na Edward Oonge walipinga wakisema “hawakupewa ushahidi huo siku saba kabla ya kesi kusikizwa waandae utetezi wao.”
Waliomba kesi iahirishwe ili wajiandae kwa mujibu wa sheria.
Mahakama ilkubaliana na mawakili hao na kusema afisi ya DPP imekaidi sheria na “kamwe haipasi kukubaliwa kuendelea na kesi kama washtakiwa hawajajiandaa.”
Hakimu aliamuru kesi hiyo iahirishwe hadi Juni 19 ndipo washtakiwa wajiandae.