Hatima ya Omanga na wenzake kujulikana wiki hii
Na CHARLES WASONGA
MASENETA watano waliojitetea mbele ya Kamati ya Nidhamu ya Jubilee kwa kukosa kuhudhurua mkutano ulioitishwa na Rais Uhuru Kenyatta katika Ikulu ya Nairobi sasa watajua hatima yao mwishoni mwa wiki hii.
Kiranja wa wengi katika Seneti Irungu Kang’ata Jumatano aliambia Taifa Leo kwamba adhabu zitakayowafika ni kama vile, kutozwa faini, kusimamishwa kwa muda au kufurushwa kutoka chama hicho.
“Kamati hiyo pia inaweza ikawasamehe wote au baadhi yao kulingana na namna walivyojitetea kuhusiana na mashtaka yaliyowakabili. Kimsingi, uamuzi wa kamati kuu utakuwa huru kwa sababu haitaingiliwa na asasi au kiongozi yeyote,” akaeleza Seneta huyu wa Murang’a.
Jumatano ilikuwa ni zamu ya Seneta Millicent Omanga na mwenzake Victor Prengei kudadisiwa na wanachama wa kamati hiyo ambapo walikariri uaminifu wao kwa Jubilee na uongozi wake.
Nao maseneta Falhada Dekow, Naomi Waqo na Mary Seneta walijitetea Jumanne.
Bi Omanga alisema hakupokea mwaliko wa mkutano huo wa Ikulu na kwamba alipata habari kuuhusu baadaye.
“Sisi kama wanasiasa hupokea jumbe nyingi zaidi kwenye simu zetu. Kwa mfano, wakati huu nimepokea zaidi ya jumbe 700. Sikupata mwaliko huo kutoka kwa kiranja wetu na hakunipigia simu kunijulisha,” akasema.
Uaminifu
Bi Omanga alisema amelipa jumla ya Sh600,000 kama ada ya kila mwezi kwa chama cha Jubilee; ishara ya uaminifu wake kwa chama hicho tawala.
Naye Bw Prengei alisema alipata habari kuhusu mkutano huo akiwa nyumbani kwao ambako kuna matatizo ya mawasiliano ya simu.
“Siku hiyo nilikuwa nyumbani kijijini. Mawimbi ya mawasiliano ya simu hayapo na barabara ni mbovu. Huwa natumia kawi ya jua lakini kwa sababu ni msimu wa mvua, simu yangu haikuwa na moto wa kutosha,” akasema.
Hata hivyo, Bw Prengei alisisitiza kuwa hajawahi kupinga miswada, hoja au maamuzi ya Jubilee katika Seneti tangu 2017.