Hatimaye Uhuru akiri magazeti si ya 'kufungia nyama'
Na LEONARD ONYANGO
KWA mara ya kwanza Rais Uhuru Kenyatta ametambua mchango wa vyombo vya habari na mashirika ya kijamii katika vita dhidi ya ufisadi.
Rais Kenyatta Jumatano alliwataka Wakenya kufichua visa vya ufisadi kupitia magazeti, runinga au redio iwapo maafisa wa Idara ya Upelelezi (DCI) watazembea kufuatilia ripoti hizo.
“Wasilisheni ripoti kuhusu visa vya ufisadi katika afisi za uchunguzi wa jinai zilizoko katika maeneo yenu. Kama hawatawasikiza, wasilisha ripoti hiyo kwa afisi za Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) iliyoko karibu,” akasema Rais Kenyatta.
“Ikiwa hawatawasikiza, toa habari kwa waandishi wa habari na kwa wanaharakati wa mashirika ya kijamii ili kuwatambulisha wahalifu hawa. Msichoke kufanya yale yaliyo sawa na yanayostahili,” akasema Rais Kenyatta.
Mara baada ya kuchaguliwa kuongoza nchi muhula wa kwanza mnamo 2013, Rais Kenyatta na naibu wake William Ruto walisema magazeti hayana manufaa na kazi yake kuu ni ‘kufungia chama’.
Mnamo Februari, mwaka huu, Rais Kenyatta alitimua wanahabari wakati wa uzinduzi wa kongamano la maafisa wa polisi jijini Nairobi.
“Sasa na nyinyi si mzime hiyo mavitu yenyu na muende. Kazi imekwisha,” akasema Rais Kenyatta.
Serikali ya Rais Kenyatta imekuwa ikabiliana na mashirika ya kijamii mara kwa mara. Katika muhula wa kwanza wa Rais Kenyatta, akaunti za benki za mashirika kadhaa ya kijamii zilifungwa huku mengine yakipokonywa leseni.