• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 11:35 AM
Hatimaye wakulima kulipwa Sh1.4 bilioni za mahindi

Hatimaye wakulima kulipwa Sh1.4 bilioni za mahindi

Na PETER MBURU

SERIKALI imetangaza kuwa itaanza kuwalipa wakulima deni la Sh3.5 bilioni, ikijitetea kuwa kuchelewesha malipo kulitokana na malalamishi kuwa kulikuwa na matapeli waliotaka kulia jasho la wakulima na hivyo ikaamua kuchunguza kwanza.

Waziri wa Ugatuzi Eugene Wamalwa Jumatatu alisema kuwa baada ya timu ya mashirika tofauti ya serikali yakiongozwa na tume ya maadili na kupambana na ufisadi (EACC) kuchunguza na kubaini lilipokuwa tatizo, sasa iko tayari kuwalipa wakulima.

Bw Wamalwa alisema serikali imetenga Sh1.4bilioni kwenye bajeti ya mwaka wa fedha wa 2018/19 ili wakulima walipwe, lakini akakiri kuwa inadaiwa jumla ya Sh3.5bilioni na wakulima na wafanyabiashara.

“Serikali sasa imeamua kumaliza shughuli ya kuwalipa wakulima waliokaguliwa na wanaofahamika ili kuwaondolea mateseko. Pesa zilizoko kwa sasa kulingana na bajeti ya 2018/19 ni Sh1.4bilioni,” akasema waziri huyo.

Bw Wamalwa alisema hivyo baada ya wizara yake kuchukua usimamizi wa pesa za uhifadhi wa vyakula muhimu (SFR), akiahidi ulipaji utafanywa kwa njia huru na ya haki na kwa wakulima wanaotambulika.

Shughuli ya wakulima kukaguliwa ilianza jana, huku serikali ikituma maafisa wake katika matawi 24 za NCPB nchini ili kurahisisha ukaguzi na shughuli za ulipaji wa deni hilo.

Ili kulipwa, wakulima watahitajika kuchukua fomu katika matawi waliyopeleka nafaka zao, wawe na kitambulisho, picha za pasipoti, tiketi za kuonyesha uzito wa nafaka walizowasilisha, na hati ya kuonyesha kuwa waliwasilisha nafaka (delivery note).

“Tunataka kwanza kuhakikisha kuwa wakulima wa kawaida wanalipwa kwani ndio wanaoumia zaidi. Baadaye tutawashughulikia wafanyabiashara kama waliosafirisha nafaka hizo na ambao walinunua na kuuzia NCPB,” akasema Bw Wamalwa.

Hatua ya waziri huyo ilikuja siku moja baada ya wakulima kupaza kilio chao kwa serikali, wakitaka iwalipe deni la mahindi.

Mnamo Jumapili, wakulima wa nafaka hiyo kutoka eneo la Bonde la Ufa waliishinikiza serikali kuharakisha ulipaji wa deni hilo, hata inapoendelea na uchunguzi kuhusu wafanyabiashara walioingiza mahindi kutoka nchi za nje na kuuzia bodi ya NCPB.

Wakulima hao aidha walitishia kuishtaki serikali kwa kukosa kuwalinda dhidi ya watu hao wanaoiuzia halmashauri ya NCPB mahindi kwa bei rahisi na hivyo kuwanyima soko.

“Haina haja kuwekeza katika kilimo cha mahindi wakati mahindi yanayotoka nje yamejaa nchini,” akasema mkurugenzi wa muungano wa kitaifa wa wakulima (KFA) Bw Kipkorir Menjo.

Tayari timu inayojumuisha wizara za ugatuzi, kilimo na usalama wa ndani imeundwa kuendesha shughuli ya ukaguzi ili kuhakikisha kuwa watakaolipwa ni wakulima halisi. Timu hiyo aidha inajumuisha bodi ya NCPB, idara za upelelezi na ujasusi (NIS na DCI), tume ya EACC na serikali za kaunti.

You can share this post!

Murathe: ‘Timu Tangatanga’ ikome kuzua uongo...

KURUNZI YA PWANI: Kampuni inayowafaa wanafunzi werevu...

adminleo