Hatutakubali ushoga wala usagaji hapa Kenya – Kinuthia
Na MWANGI MUIRURI
NAIBU Waziri wa Elimu Zack Kinuthia Jumatatu alisema kuwa serikali ya Kenya kamwe haitawahi kukubali shinikizo za baadhi ya mataifa ya magharibi ikubali injili za ushoga na usagaji pamoja na uavyaji mimba.
Aidha, alisema kuwa serikali haiko tayari kwa vyovyote vile kukubali ajenda ya wanaharakati wanaofadhiliwa na mataifa hayo ya Magharibi ya kupunguza umri wa maamuzi ya ngono kutoka ule wa sasa wa 18 hadi miaka 13.
Pia, serikali haiko tayari kukumbatioma elimu za ngono katika shule za msingi na sekondari akisema kuwa “hilo ni suala la ushauri wa kimalezi wala sio la silibasi.”
Alisema kuwa kumekuwa na shinikizo zinazosukumwa kwa ahadi za misaada ya kifedha “na ikiwa tutapata usaidizi ndio tunajisi imani zetu za kimila na kidini, basi tuachwe tufe na shida zetu.”
Alisema kuwa msimamo huo ni wa kiserikali na pia wake kibinafsi akiongeza kuwa taifa hili haliko tayari kumenyana na Mungu kuhusu maadili na heshima kwa uhai ambao yeye tu ndiye wa kutoa na kutwaa.
“Ningetaka kukariri hapa kama msimamo wangu binafsi na pia wa Rais Uhuru Kenyatta na serikali yake kuwa hatutawahi kujadili masuala hayo katika mabunge yetu hapa nchini na iwapo kunao wa viongozi walio na uvutio wa maovu hayo ya kiimani na kimila, basi hakuna idhini ya rais itawahi kupendekeza hayo yawe sheria ya nchi,” akasema.
Akiongea katika mji wa Kigumo, Bw Kinuthia alisema kuwa “Uafrika na dini zetu zote nchini hazina nafasi ya ndoa za waume kwa waume na wake kwa wake, uavyaji mimba na ngono za watoto kwa watu wazima.”
Alisema kuwa “serikali inajua kuna baadhi ya viongozi na wanaharakati ambao ghafla wameanza kuhubiri imani za ushoga na usagaji sambamba na uavyaji wa mimba. Hao ni makuhani wa kishetani nchini.”
Aliongeza kuwa amri ya rais kuwa kliniki zote ambazo huwapa wasichana wachanga huduma za upangaji uzazi ziandamwe, zipokonywe leseni na wahudumu wakamatwe na washtakiwe ingalipo.
Alisema kuwa amri hiyo imewasilishwa kwa makamishna wote wa Kaunti akiongeza kuwa maovu mengine yanayomulikwa katika amri hiyo ni ndoa za mapema kwa wasichana, ukeketaji na dhuluma zinginezo dhidi ya watoto.
Alisema kuwa amri hiyo ya rais ilitolewa katika kikao rasmi cha kutafuta mbinu ya kupambana na janga la wasichana wa shule kutungwa mimba, kuathirika katika visa vya uavyaji mimba na ngono kiholela.
“Tumekubali kuwa tuko na janga la wasichana wetu wachanga kuwa katika maovu ya ngono. Hatuwezi tukaficha vichwa vyetu mchangani na kujipa imani kuwa mambo yatakuwa sawa. Tuko na shida ndio na ni lazima tukabiliane nayo kimasomaso,” akasema.
Alisema kuwa rais amesisitiza kuwa upangaji uzazi unakubalika tu kati ya waliokomaa kiumri na pia wale walio katika ndoa.
“Sasa tunataka kujua kliniki yako inatoa huduma za upangaji uzazi kwa watoto ndio wapange nini na wakiwa na nani…Tunataka kujua wewe ukiwa na Kliniki yako kwa kuwa umekomaa miaka ya kutambua lililo halali na haramu ni uwazimu gani umekukumba ndio uzindiue harakati za kibiashara za kuharibu watoto wa taifa hili,”akasema.
Alisema kuwa huduma ambazo wasichana hao hupokezwa katika kliniki hizo haramu ni sindano za kusimamisha ratiba ya hedhi, matembe ya kuua shime (spamu), mipira ya kondomu ya kike na pia tembe za dharura za kuzuia uja uzito.
“Hiyo ni biashara sawa na kuuza gurunedi. Ni uhaini usio na kifani kwa wanataaluma. Tunajua kuwa hata kuna wazazi ambao hugharamia huduma hizo kwa msingi wa kujaribu kuhepa aibu ya binti zao kupata uja uzito. Si utoe ushauri mwafaka wa kimalezi badala ya kumwonyesha mtoto wako njia ya kushiriki ngono bila hofu yoyote ya kushika mimba?” akahoji.
Bw Kinuthia alisema kuwa wazazi wa aina hiyo husahau kuwa kuna hatari zingine ndani ya utumizi wa mbinu za upangaji uzazi kwa walio wa umri wa chini, zikiwemo maambukizi ya magonjwa na pia kuzuka kwa utasa au kuzaa viwete.