Hesabu ya Dola yakosa kumfanya aachiliwe mapema
ALIYEKUWA mwanahabari Moses Dola Otieno, ambaye anatumikia kifungo jela kwa mauaji ya mkewe, amepoteza ombi lake la kutaka muda wa kukaa rumande kuzingatiwa katika kifungo chake cha miaka 10.
Hii ni baada ya Jaji wa mahakama Kuu ya Nakuru, Hedwig Ong’udi kutupilia mbali ombi lake ambalo alitaka tarehe yake ya kuachiliwa kutoka jela iwe mapema baada ya kuzingatiwa kwa muda wa miezi 21 alizokaa rumande kabla ya kulipa dhamana.
Dola alihukumiwa kutumikia kifungo cha miaka 10 jela mnamo Novemba 29, 2018, baada ya kukiri kosa la kuua bila kukusudia kufuatia makubaliano na upande wa mashtaka.
Alikiri kumuua mkewe Sarah Wambui Kabiru, ambaye pia alikuwa mwanahabari mnamo Mei 3, 2011 nyumbani kwao Nairobi.
Katika ombi lake lililowasilishwa Septemba 2023, Dola alitaka amri ya mahakama ya kuachiliwa kwake mapema baada ya kuzingatia muda aliokaa rumande na muda ambao tayari ametumikia gerezani pamoja na msamaha.
Kulingana na hesabu yake, wakati anaotarajia kuachiliwa unapaswa kuwa Novemba 2023 badala ya 2025.
Hii ni baada ya kuhesabu miezi 21 aliyokaa rumande, miaka minne aliyokaa gerezani na msamaha ambao kwa mujibu wake unapaswa kuwa thuluthi moja ya kifungo chake.
Hesabu yake inaonyesha kuwa alikuwa ametumikia siku 27 zaidi kinyume cha sheria wakati wa kuwasilisha ombi ambazo alitaka kulipwa fidia.
Alidai kubaguliwa na mahakama iliyomhukumu kwa kukosa kuzingatia muda aliokaa rumande.
Hata hivyo, Jaji Ong’udi katika uamuzi wake aligundua kuwa Dola alikuwa amewasilisha maombi sawa na hayo mbele ya Mahakama Kuu ya Nairobi akitaka afueni sawa na hiyo lakini yakatupiliwa mbali.