Hii ndiyo sababu ilinibidi nikutane na Ruto – Oparanya
Na BENSON AMADALA
GAVANA wa Kakamega Wycliffe Oparanya amefafanua sababu za kukutana na Naibu Rais William Ruto Jumatano iliyopita.
Bw Oparanya, ambaye alihutubu katika hafla ya makaribisho ya mbunge wa Lurambi Titus Khamala, alisema kuwa alikuwa akijaribu kumshinikiza Bw Ruto kutupilia mbali azima yake ya kuwania urais, na badala yake kumuunga mkono mwaniaji kutoka jamii ya Abaluhya mnamo 2022.
Bw Oparanya amekuwa akihusishwa na mikakati ya kuwa mgombea-mwenza wa Bw Ruto katika uchaguzi huo. Alieleza kuwa, kiini kikuu cha mkutano wao kilikuwa kujadili mwelekeo wa kisiasa kuhusiana na uchaguzi huo.
Vile vile, alisema kwamba alimwomba mbunge huyo kuandamana naye, lakini kulizuka kizaazaa alipowasili.
Gavana huyo aliwasili muda mfupi baada ya kiongozi wa Chama cha Amani (ANC) Musalia Mudavadi, ambaye ndiye alikuwa mgeni mheshimiwa.
Bw Mudavadi na viongozi wengine walikuwa washaondoka, wakati Bw Oparanya na ujumbe wake walipowasili.
Bw Ruto, aliyekuwa ameombwa kuhutubia mkutano huo pia alikuwa ashaondoka kuhudhuria hafla nyingine.
Bw Oparanya aliwasili akiwa ameandamana na Seneta wa Kakamega Cleophas Malala. Baadhi ya wananchi waliohudhuria walianza kuondoka, lakini kikosi chake cha mawasiliano kikaweka kipaaza ili kumwezesha kuhutubia umati huo.
“Wakati Naibu Rais aliponialika, nilimwomba Bw Khamala kuandamana nami ili kuondoa madai yoyote kuhusu mkutano wetu,” akasema.
Hata hivyo, hakueleza mahali mkutano huo ulipofanyikia, wala yale walikubaliana.
“Kwa sasa, lengo langu ni kuwashinikiza viongozi wa Abaluhya kuungana ili kumuunga mkono mmoja wetu kuwania urais mnamo 2022,” akasema Bw Oparanya.
Alimlaumu Bw Mudavadi na kiongozi wa Ford-Kenya Moses Wetang’ula kuhusu mpango wao wa kubuni muungano wa kisiasa kufikia 2022.
“Sipingi kiongozi yeyote wa Waluhya kuwania urais mnamo 2022, ila Mabw Mudavadi na Wetang’ula wanapaswa kukoma kuipotosha jamii hiyo kuhusu muungano wao wa kisiasa,” akasema.
Kiongozi huyo alisema kuwa wawili hao wanapaswa kuwahusisha viongozi wengine katika mkakati huo, ikiwa wanalenga kuirai jamii hiyo kuwaunga mkono.
Alikosoa mpango wao, akisema utakuwa sawa na kupoteza muda, kwani itabidi jamii hiyo kuungana na zingine ili kutwaa urais.
Alimrai Bw Khalwale kukoma kumkashifu kiongozi wa ODM Raila Odinga kuhusu muafaka wake wa kisiasa na Rais Uhuru Kenyatta.
“Bw Khalwale anapaswa kukoma kumtusi Bw Odinga katika mikutano ya kisiasa, kwa kuwa wako katika viwango tofauti sana vya kisiasa,” akasema.
Kumekuwa na mijadala kuhusu mikakati itakayoiwezesha jamii hiyo kutwaa urais mnamo 2022, huku viongozi mbalimbali wakihimiza umuhimu wa kuungana kisiasa.
Majuzi, Waziri wa Maji Eugene Wamalwa alisisitiza kuwa ni kupitia umoja wake ambapo wataibuka washindi.
Wakati huo, alitangaza kuzika tofauti zake za muda mrefu na Kiongozi wa Ford Kenya Moses Wetang’ula.